Yondani avutwa Simba

07Apr 2020
Adam Fungamwango
Nipashe
Yondani avutwa Simba
  • ***Tshabalala amjumuisha kikosini, pia aelezea bao lake bora kabisa huku akiliacha lile la..

Wakati beki wa kati wa Yanga, Kelvin Yondani, akiwa miongoni mwa wachezaji wa timu hiyo waliokosa namba ya kudumu katika kikosi cha kwanza cha Kocha Mbelgiji Luc Eymael, beki wa kushoto wa Simba, Mohamed Hussein 'Tshabalala', ametuma ujumbe kwa viongozi na benchi la ufundi la mabingwa hao ...

watetezi wa Ligi Kuu Bara kuwa anafaa kurejeshwa Msimbazi.

Yondani kwa sasa amekuwa hana namba ya kudumu kwenye kikosi cha Yanga chini ya Eymael na hata mashabiki wa timu hiyo wameonekana hawana wasiwasi tena pindi anapokosekana uwanjani kutokana na kiwango cha kuvutia kinachonyeshwa na Mghana Lamine Moro.

Akizungumza katika kipindi cha kuchati na mashabiki, kwenye channel inayorushwa na klabu ya Simba, Tshabalala alitaja kikosi chake bora huku kikiundwa na wachezaji karibuni wote wa timu yake ya Simba kasoro Yondani wa Yanga na Aboubakara Salum 'Sure Boy' wa Azam FC.

Aliowataja kutoka Simba ni Aishi Manula, Shomari Kapombe, yeye mwenyewe, Yondani na Erasto Nyoni, Jonas Mkude, Clautos Chama, Meddie Kagere, John Bocco na Ibrahim Ajibu.

Tshabalala alisema kuwa kati ya mawinga hatari ambao amewahi kukutana nao ni Simon Msuva, mchezaji wa zamani wa Moro United na Yanga, ambaye kwa sasa anacheza soka la kulipwa nchini Morocco katika klabu ya Difaa Hassani El Jadidi.

"Hata wachezaji wenzangu niliokuwa nacheza nao kina Hassan Isihaka, siku tunakwenda kucheza nao, wananiambia kalale mapema, ujiandae kwa sababu kesho una shughuli pevu na Msuva na kweli 'kinachimbika', mmoja ni lazima siku hiyo asalimu amri, iwe mimi au yeye," alisema.

Alimtaja mchezaji aliyemvutia zaidi hadi kufuata nyayo zake na kuiga staili zake za uchezaji ni Issa Rashid 'Baba Ubaya', ambaye aliwahi kuichezea Simba mwaka 2013, akitokea Mtibwa Sugar, lakini alicheza kwa misimu miwili kabla ya kurejea tena Mtibwa hadi sasa.

"Nilikuwa namfuatilia sana, kusema kweli niliiga vitu vingi kutoka kwake, wakati huo mimi niko kwenye akademi ya Azam FC, baadaye nikaenda Kagera Sugar, lakini kuna wakati fulani nikabahatika kucheza naye Simba," alisema mchezaji huyo ambaye pia anaichezea timu ya Taifa ya Tanzania, Taifa Stars.

Kuhusu wakati wake bora kabisa kwenye soka, alisema kuwa ni ule ambao timu yake ya Simba ilifanikiwa kutinga hatua ya robo fainali ya Ligi ya Mabingwa Afrika msimu uliopita.

Katika hali isiyokuwa ya kawaida, ikidhaniwa kuwa goli lake bora angeweza kulitaja lile la kusawazisha dhidi ya AS Vita ya DR Congo, Simba ikishinda mabao 2-1, Tshabalala alisema bao lake bora ambalo hatolisahau ni lile alilofunga dhidi ya Kagera Sugar, Septemba 26, mwaka jana, Simba ikishinda kwa mabao 3-0 kwenye Uwanja wa Kaitaba mjini Bukoba.

"Ni kwa sababu nilitumia akili sana kufunga; niliuchukua mpira nikawaacha mabeki, nikaingia ndani, nikampa Kagere, akanirudishia kwenye njia, nikaenda kufunga," alisimulia mithili ya mtangazaji.

Alipoulizwa kama siku moja anaweza kuwa kocha wa mpira wa miguu, alikataa na kusema kama akifanya kazi hiyo, ataishusha daraja timu anayoifundisha.