Zanzibar walilia Daraja la Kwanza

07Jul 2020
Hawa Abdallah
Zanzibar
Nipashe
Zanzibar walilia Daraja la Kwanza

WADAU wa soka Zanzibar wameiomba serikali kuruhusu kuendelea kwa mechi za Ligi Daraja la Kwanza ili kupata timu zitakazopanda daraja kuelekea msimu mpya wa Ligi Kuu Zanzibar 2020/21, imeelezwa.

RAIS WA ZANZIBAR, DR ALI MOHAMMED SHEIN:PICHA NA MTANDAO

Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar iliruhusu kuendelea kwa Ligi Kuu tu huku ligi nyingine zikisubiri mwongozo mpya wakati huu bado janga la corona haijamalizika nchini.

Katibu wa Kilimani City inayoshiriki Ligi Daraja la Kanda ya Unguja, Abdulrahman Salum, alisema kwa niaba ya wenzake, serikali iangalie tena uamuzi wa kuruhusu ligi nyingine ili kukamilisha msimu huu na hatimaye kupata timu zitakazopanda daraja kwa haki.

Salum alisema Ligi Daraja la Kwanza Kanda ya Unguja ilikuwa imebakisha michezo michache na anaamini ikiruhusiwa tena, watatumia wiki mbili kukamilisha msimu huu huku wakiahidi kufuata mwongozo wa Wizara ya Afya kama inavyotekelezwa katika Ligi Kuu Zanzibar.

“Tunajua serikali inafanya hivi kutokana na kuendelea kujikinga na virusi vya corona, hususani katika zile sehemu ambazo mikusanyiko ya watu inakuwapo , tunawaomba pia waruhusu Ligi Daraja la Kwanza ikaendelea na ikasisitiza taratibu zote za kujikinga na corona zikafuatwa," Salum alisema.

Jumla ya timu 18 zinashiriki Ligi Daraja la Kwanza Kanda ya Unguja ambayo itashusha klabu nne huku klabu 14 za Pemba zinachuana katika ligi hiyo itakayoshusha timu sita.

Habari Kubwa