Afcon 'laivu' DStv Bomba, Diamond kukinukisha

12Jan 2017
Lasteck Alfred
Nipashe
Afcon 'laivu' DStv Bomba, Diamond kukinukisha

WAKATI DStv ikiamua kuonyesha michuano ya Afcon 2017 kupitia kifurushi chake cha bei nafuu cha Bomba, Wizara ya Habari,

Wizara ya Habari, Utamaduni Michezo na Sanaa ikishirikiana na kampuni hiyo imemkabidhi bendera ya taifa pamoja na tiketi sita mwanamuziki wa kizazi kipya nchini, Naseeb Abdul 'Diamond Platnumz' kwa ajili ya kwenda kufanya shoo katika ufunguzi wa michuano hiyo, Gabon.

Diamond ni miongoni mwa wasanii teule watakaotumbuiza katika hafla hiyo, kitendo ambacho kimechukuliwa na Watanzania wengi kuwa ni fursa ya Tanzania kusikika katika mashindano hayo, licha ya timu yetu kutofuzu.

Waziri wa Habari, Utamaduni, Michezo na Sanaa, Nape Nnauye alisema kuwapo kwa Diamond kwenye uzinduzi wa michuano hiyo ni kitendo cha kujivunia na kwamba serikali ikishirikiana na DStv imefanya jitihada kubwa kufanikisha safari ya WCB kuelekea Gabon.

Kwa upande wake Diamond aliishukuru serikali na DStv kwa ushirikiano wao hususan kufanikisha safari yao ya kuelekea Gabon.

Aliongeza kuwa jitihada binafsi za waziri wa habari ziliwezesha mchakato huo kufanikiwa na kwamba wanaahidi kuwa hawaendi kama WCB, bali kama Watanzania na watahakikisha kuwa wanaipeperusha vema bendera ya Tanzania katika onyesho hilo litakalofanyika kesho kutwa, Jumamosi.

Michuano ya AFCON ya mwaka huu inanogeshwa zaidi na uwapo wa wachezaji nguli ulimwenguni hususan wale wanaochezea klabu kubwa kama Manchester United, Arsenal, Chelsea, Liverpool, Dortmund nyingine kubwa duniani.

Wakali kama Mohamed Elneny, Eric Bailly, John Obi Mikel, Pierre Aubemayang, Riyad Mahrez, Sadio Mane na Victor Moses ni miongoni mwa vigogo watakaoonyesha umahiri wao katika michuano hiyo.

Kaimu Mkurugenzi Mtendaji wa Multichoice Tanzania, Salum Salum, ametanabahisha kuwa kwa kuwa DStv ndicho king’amuzi pekee kitakachoonyesha michuano hiyo mubashara 'laivu' kupitia chaneli yake ya michezo ya SuperSport4 (DStv 204), wameamua kuiweka michuano hiyo kwenye kifurushi cha bei nafuu kabisa cha Bomba, ili kuwawezesha Watanzania wengi zaidi kuiona michuano hiyo moja kwa moja, ambayo itaanza kutimua vumbi Januari 14 na fainali itakuwa Februari 05 mwaka huu.

Habari Kubwa