Afcon yamkataa Kapombe, aumia

04Jun 2019
Somoe Ng'itu
DAR
Nipashe
Afcon yamkataa Kapombe, aumia

WAKATI mshambuliaji wa Timu ya Taifa (Taifa Stars), John Bocco, amewataka wadau wa soka nchini kukiamini kikosi cha timu hiyo ambacho kinajiandaa na fainali za Kombe la Mataifa ya Afrika (Afcon 2019), beki wa kulia, Shomary Kapombe ameumia tena akiwa na kikosi hicho.

Shomary Kapombe.

Awali Kapombe aliumia akiwa katika kikosi cha Stars kilipokuwa nchini Lesotho mwaka jana na majeraha hayo yalimfanya akae nje kwa muda mrefu na kushindwa kuitumikia ipasavyo klabu yake ya Simba iliyomrejesha akitokea Azam FC.

Meneja wa Stars, Danny Msangi, aliliambia gazeti hili jana kuwa Kapombe alijitonesha mwenyewe juzi wakati akifanya mazoezi yake binafsi.

"Ni kweli ameumia, amejitonesha mwenyewe akiwa hotelini wakati akiendelea na programu zake binafsi za mazoezi, leo (jana) hata mazoezini hajatokea kabisa," alisema kwa kifupi meneja huyo.

Akizungumza baada ya mazoezi ya jana asubuhi, Bocco, alisema kuwa kila mchezaji anataka kufanya vizuri kwa sababu wanafahamu ni nafasi nyingine ya kujitangaza kimataifa.

Bocco alisema: "Mazoezi yanakwenda vizuri, tunajua huko mambo yatakuwa si rahisi, ila mpira una matokeo mazuri na vile vile una matokeo yanayoumiza, tunajiandaa ili twende tukapambane, hatuna wasiwasi kwa sababu wote tuna nafasi sawa."

Naye beki wa kushoto wa timu hiyo, Gadiel Michael anayetokea Yanga, alisema: "Kupata nafasi hii kwangu ni jambo ambalo lilikuwa ninaliwaza sana, ni ndoto ambayo nilikuwa nayo kwa muda mrefu, tutaenda huko kupambana kwa sababu tunajua ni fursa nyingine ya kujiuza, mawakala na watu mbalimbali watakuwapo huko kufuatilia wachezaji."

Habari Kubwa