Africarriers yaipa Simba mabasi 3

25Sep 2021
Saada Akida
Dar es Salaam
Nipashe
Africarriers yaipa Simba mabasi 3

KATIKA kuendelea kujiimarisha kiuchumi, Kampuni ya magari ya Africarriers imeingia mkataba wa udhamini wa miaka minne na mabingwa wa Ligi Kuu Tanzania Bara, Simba, wenye thamani ya Sh. milioni 800.

Ofisa Mtendaji Mkuu wa Simba, Barbara Gonzalez, alisema jana jijini Dar es Salaam kupitia mkataba huo, klabu yao itapata vitu mbalimbali kutoka kwa wadhamini hao.

Barbara alitaja baadhi ya vitu ambavyo Simba itapata ni pamoja na basi aina ya Golden Dragon lenye uwezo wa kubeba watu 60, basi lingine aina ya Eicher lenye uwezo wa kubeba watu 45 na basi dogo aina ya Coaster.

"Basi kubwa litatumiwa na timu ya wakubwa, la watu 45 litatumiwa na Simba Queens na Coaster litatumiwa na timu ya vijana," alisema Barbara.

Mkuu wa Idara ya Sheria wa Africarriers, Ngassa Mboje, alisema pia kampuni hiyo itakuwa wadhamini wa mavazi wa timu ya vijana ya Simba.

"Ni jambo la fahari kwetu kuanza uhusiano huu na mabingwa wa kihistoria wa Tanzania. Tunaamini pande zote mbili zitanufaika na uhusiano huu," alisema Mboje.

Mkataba huo na Africarriers ni watatu kuingiwa na mabingwa hao mara nne mfululizo wa Ligi Kuu Tanzania katika kipindi cha mwezi mmoja.

Tayari Wekundu wa Msimbazi wameingia mikataba na Air Tanzania kwa ajili ya kuwasafirisha kwenye safari za ndani na nje ya nchi pamoja na Emirates itakayotoa tuzo kwa wachezaji watakaofanya vyema kila mwezi.

Wadhamini wakuu wa Simba ambao ndio klabu pekee Tanzania iliyobakia kwenye mashindano ya kimataifa ya Ligi ya Mabingwa Afrika ni SportPesa.