Aiyee: Mlango upo wazi Simba, Yanga

10Jun 2019
Na Mwandishi Wetu
Nipashe
Aiyee: Mlango upo wazi Simba, Yanga

BAADA ya kufanikiwa kuibakiza Mwadui FC Ligi Kuu Tanzania Bara, mshambuliaji tegemeo wa timu hiyo ya Shinyanga, Salim Aiyee, amesema milango iko wazi kwa Simba, Yanga na klabu za nje ya nchi kufanya naye mazungumzo kwa ajili ya kumsajili.

Salim Aiyee.

Aiyee ambaye alifunga mabao 17 msimu wa Ligi Kuu Tanzania Bara uliomalizika hivi karibuni, juzi alicheka na nyavu mara mbili katika ushindi wa 2-1 dhidi ya Geita Gold FC na kuiwezesha klabu yake ibakie katika ligi hiyo ya juu nchini.

Akizungumza na gazeti hili jana, Aiyee, alisema amepokea ofa mbalimbali, lakini bado hajaridhishwa na dau alilopewa, hivyo ataendelea kujihesabu yeye ni mchezaji wa Mwadui FC.

Aiyee alisema anakiamini kiwango chake na kwa sasa hana haraka ya kufanya uamuzi wa kusajili mpaka pale atakavyoona, amepata dau linalomridhisha.

"Kuondoka ni mapenzi ya Mungu, sisi wacheza mpira ni kama wafanyabiashara, kama itakuja klabu na hela nzuri, basi nitakwenda, nina ofa nyingi kutoka klabu za ndani na nje ya Tanzania, lakini bado hawajafikia kiwango cha pesa ninachokitaka," alisema Aiyee.

Aliongeza kwamba hatakiwi pia kuona anakwenda katika timu ambayo haitaendeleza kipaji chake, kwa sababu bado ana ndoto za kusonga mbele katika mchezo huo.

"Naamini nitapata timu nzuri na bora ya kuitumikia kwa ajili ya msimu ujao, sitaki kufanya uamuzi wa haraka, ila kama nitakosa, nitabakia hapa Mwadui, kwangu ni kama nyumbani, ingawa mimi ni mtu wa Tanga, ila kipaji changu kimeonekana kupitia hapa Mwadui," Aiyee aliongeza.

Mwadui FC na Kagera Sugar iliyoshinda mabao 2-0, zimebakia katika ligi hiyo baada ya kushinda mechi zao za marudiano za mchujo 'Play off' na kuzifanya Geita Gold na Pamba kuiendelea kubaki Ligi Daraja la Kwanza msimu ujao.

Habari Kubwa