Ajib kujaribiwa Jomo Cosmos

11May 2016
Somoe Ng'itu
Dar es Salaam
Nipashe
Ajib kujaribiwa Jomo Cosmos
  • ...Nyota huyo alisajiliwa na Simba baada ya kuonyesha uwezo wa juu akiwa na timu ya vijana (Simba B) atafanya majaribio katika timu zaidi ya tatu akiwa Afrika Kusini...

MSHAMBULIAJI wa Simba, Ibrahim Ajib jana alitarajiwa kuanza majaribio katika klabu ya Jomo Cosmos inayoshiriki Ligi Kuu ya Afrika Kusini imeelezwa jana.

mshambuliaji wa simba ibrahim ajib akimtoka beki wa tanzania prisons.

Taarifa zilizopatikana kutoka kwa wakala wa mchezaji huyo (jina tunalihifadhi) zilisema kuwa Ajib ataanza kufanya majaribio na timu hiyo kutokana na benchi la Kaizer Chiefs kukosa nafasi ya kumfuatilia straika huyo kwa sasa.

Chanzo hicho kiliongeza kuwa mbali na Jomo Cosmos, Ajib pia atatafutiwa nafasi ya kufanya majaribio katika klabu nyingine za ligi hiyo ili kujaribu kuonyesha uwezo wake.

"Alifika salama na tayari wakala wake anaendelea na mazungumzo na timu zaidi ya tatu ili kumpatia nafasi ya kufanya majaribio, tunaamini hiyo itamsaidia kupata timu haraka," kilisema chanzo chetu.

Habari zaidi zinaeleza kuwa baadhi ya viongozi walikuwa wanafahamu safari ya mchezaji huyo tofauti na ilivyodhaniwa kuwa ametoroka.

"Hii safari ya Ajib inafanana na ile ya Kazimoto, baadhi ya viongozi wanafahamu kilichokuwa kinaendelea," kilisema chanzo chetu.

Ajib ambaye mkataba wake unaisha mwisho wa msimu aliachwa jijini kutokana na kutumikia adhabu ya kadi nyekundu aliyoonyeshwa katika mechi dhidi ya Mwadui FC ambayo Simba ililala 1-0.

Habari Kubwa