Ajibu afunguka, Matola awaonya

14Mar 2019
Na Waandishi Wetu
Dar es Salaam
Nipashe
Ajibu afunguka, Matola awaonya

WAKATI vinara wa Ligi Kuu Tanzania Bara, Yanga ya jijini Dar es Salaam wakitamba wanakwenda Iringa kwa kazi moja ya kuchukua pointi tatu ingawa wanafahamu wazi mchezo wao dhidi Lipuli FC hautakuwa mwepesi, kocha wa wenyeji wao hao, Selemani Matola amewataka mashabiki kujitokeza kwa wingi katika ....

Uwanja wa CCM Samora Jumapili kushuhudia wakifanya kweli.

Akizungumza na gazeti hili jana, nahodha wa Yanga, Ibrahim Ajibu, alisema kuwa timu yao ina "kiu" ya kuchukua ubingwa wa ligi hiyo ili waweze kutimiza malengo yao na wanafahamu hawatakiwi kupoteza tena pointi.

Ajibu alisema kuwa kila mchezaji wa Yanga ambaye atapata nafasi ya kucheza, anafahamu mipango iliyowekwa na benchi la ufundi, klabu na timu yote kwamba wanahitaji matokeo ya ushindi na si kitu kingine.

"Tunajua walioko nyuma watatukimbiza, hakuna ambaye anafurahi kuona tunaongoza ligi kwa muda mrefu, ingawa baadhi ya timu kama Simba zimecheza mechi chache, hiyo hatuiangalii, tunachoangalia ni kufanya vizuri katika kila mechi tutakayocheza," alisema Ajibu.

Mshambuliaji huyo aliongeza kuwa kila mchezaji anatakiwa kujituma katika dakika zote atakazokuwa uwanjani na kwao neno kukata tamaa halipo.

Naye Meneja wa Yanga, Hafidh Saleh, alisema kuwa kikosi cha timu hiyo kinatarajia kuelekea Iringa leo, huku wakiwa na tahadhari ya kuwavaa Lipuli.

Lakini wenyeji wao, Lipuli wametamba kuwa wamejipanga kuibuka na ushindi katika mchezo huo dhidi ya Yanga na hiyo ni kauli ya Kocha wa timu hiyo, Matola.

"Sisi benchi la ufundi tumelifanyia kazi jambo hilo na sasa tunajipanga kuhakikisha tunaibuka na ushindi katika uwanja wetu wa nyumbani," alisema Matola.

Matola alisema mechi dhidi ya Yanga ni ngumu lakini watacheza kufa au kupona ili kufuta uteja wa bao moja walilofungwa katika mchezo wa raundi ya kwanza jijini Dar es Salaam.

Imeandikwa na waandishi wetu Somoe Ng'itu Dar na Friday Simbaya, Iringa

Habari Kubwa