Ajibu ainyima usingizi Yanga

11Jun 2019
Somoe Ng'itu
Dar es Salaam
Nipashe
Ajibu ainyima usingizi Yanga
  • ***Yamweka kitako kisa mkataba Simba, atoa matumaini akiitaka...

UONGOZI wa Yanga ya jijini Dar es Salaam umesema bado unahitaji huduma ya nahodha na mshambuliaji wao, Ibrahim Ajibu, ambaye anatajwa kusaini mkataba wa awali na mabingwa wa Ligi Kuu Tanzania Bara, Simba, imefahamika.

Ibrahim Ajibu.

Taarifa katika mitandao mbalimbali ya kijamii jana zilieleza kuwa Ajibu amesaini mkataba mpya wa miaka miwili, jambo ambalo si kweli.

Akizungumza na gazeti hili jana, kiongozi mmoja wa juu (jina tunalihifadhi), alisema bado mshambuliaji huyo hajasaini mkataba mpya na wanaendelea kumshawishi ili akubali kubakia katika klabu hiyo.

Kiongozi huyo alisema wameshafanya vikao mbalimbali na mshambuliaji huyo, lakini hawakufanikiwa kukamilisha mazungumzo ya kusaini mkataba mpya.

"Tunamhitaji sana, ni mchezaji ambaye mchango wake kwetu ni muhimu, tulimfuata kambini Stars Whitesands, tukazungumza naye tukiwa viongozi watatu, lakini hatukumaliza mchakato huo uliotupeleka," kilieleza chanzo chetu.

Aliongeza kuwa mara zote, Ajibu ambaye ametemwa katika kikosi cha Taifa Stars kilichokwenda kwenye fainali za Kombe la Mataifa ya Afrika (Afcon) amekuwa akiwaambia mabosi wa Yanga wasiwe na wasiwasi, atasaini mkataba mpya muda ukifika.

"Kila tukiongea naye (Ajibu), anatupa matumaini, anatuambia hatuwezi kushindwana mabosi wangu," aliongeza kwa kifupi kiongozi huyo.

MUSONYE AWAPONDA

Katibu Mkuu wa Baraza la Soka Afrika Mashariki na Kati (Cecafa), Nicholas Musonye, ameziponda klabu za Simba na Yanga kwa uamuzi wao wa kujitoa katika mashindano ya Kombe la Kagame ambayo yanatarajiwa kufanyika kuanzia Julai 7 hadi 21, mwaka huu jijini Kigali, Rwanda.

Musonye alisema klabu hizo zinapoteza fursa ya kujiimarisha kuelekea msimu mpya, na hiyo kuzifanya zishindwe kufika mbali katika mashindano ya Ligi ya Mabingwa na Kombe la Shirikisho Afrika.

"Viongozi wao ni bure kabisa, timu maana yake ni kushiriki mashindano, huwezi kuwa imara kama huchezi, hushindani, au hujiandai vema," alisema Musonye.

Licha ya kuukosa ubingwa wa Ligi Kuu, Yanga itashiriki mashindano ya Ligi ya Mabingwa Afrika pamoja na Simba baada ya Shirikisho la Soka Afrika (Caf) kuipa Tanzania Bara nafasi nne katika mashindano yake ya msimu ujao.

Habari Kubwa