Ajibu 'atia doa' shughuli Yanga

07Aug 2018
Faustine Feliciane
DAR ES SALAAM
Nipashe
Ajibu 'atia doa' shughuli Yanga

WAKATI kikosi cha Yanga kikiwa Morogoro kujiandaa na mchezo wake wa kimataifa pamoja na Ligi Kuu Tanzania Bara, mshambuliaji nyota wa timu hiyo, Ibrahim Ajibu, hajaripoti kambini, imeelezwa.

Ibrahim Ajibu.

Ajibu hajajiunga na wenzake kwa kile kilichoelezwa kusumbuliwa na Malaria.

Mratibu wa timu hiyo, Hafidh Saleh, alisema wachezaji wote wanaendelea vema na mazoezi, lakini Ajibu bado hajaungana na wenzake kwa kuwa ni mgonjwa.

"Wachezaji wote wapo na wanaendelea vizuri na mazoezi, ila Ajibu bado hajafika kambini na taarifa iliyopo ni kwamba anaumwa Malaria," alisema Saleh.

"Sifahamu lini atakuja ila kocha Zahera anaendelea na program yake ya mazoezi..., tunafanya mazoezi mara mbili kwa siku," aliongeza kusema.

Alisema Zahera alipenda kuona wachezaji wake wote wawepo kambini ili kurahisisha program yake.

Hata hivyo, Ajibu hakupatikana jana kuelezea hali yake na lini ataungana na wenzake wakati huu kikosi hicho cha Yanga kikiwa kimeweka kambi ya wiki mbili mkoani humo.

Habari Kubwa