Ajibu: Sababu kipigo Yanga

21Jan 2019
Na Mwandishi Wetu
Nipashe
Ajibu: Sababu kipigo Yanga

MSHAMBULIAJI na nahodha wa Yanga, Ibrahim Ajibu, amesema hakuna mtu wa kulaumiwa kufuatia kipigo cha bao 1-0 walichokipata kutoka kwa Stand United juzi.

MSHAMBULIAJI na nahodha wa Yanga, Ibrahim Ajibu.

Wakiwa kwenye Uwanja wa Kambarage juzi, Yanga walipokea kipigo hicho cha kwanza msimu huu kwenye Ligi Kuu na kuhitimisha rekodi yao ya kucheza michezo 19 bila kufungwa.

Ajibu alisema katika mchezo huo walitengeneza nafasi nyingi, lakini hawakuwa makini kuzitumia wakati wapinzani wao walipata nafasi na kuitumia vizuri.

"Tumefungwa kimchezo hakuna wa kumlaumu... kocha atakuwa kaona makosa yetu, tunaenda kuyafanyia kazi," alisema Ajibu.

Aidha, alisema kila wanapomaliza mchezo mmoja wanajipanga kwa michezo inayofuata, hivyo wanasahau matokeo hayo na wanaelekeza nguvu kwenye michezo mingine.

Baada ya mchezo huo wa juzi, Yanga sasa wanarejea Dar es Salaam kujiandaa na michuano ya Sportpesa Cup inayotarajiwa kuanza kesho.

Hata hivyo, matokeo ya juzi bado yanaendelea kuiweka Yanga kileleni mwa msimamo wa ligi hiyo ikibakiwa na pointi zake 53 ikifuatiwa na Azam yenye pointi 47.

Habari Kubwa