Ajibu: Ubingwa ni wa Simba

09Feb 2016
Shinyanga
Nipashe
Ajibu: Ubingwa ni wa Simba

BAADA ya kushinda mechi zote sita zilizopita za Ligi Kuu ya Vodcaom Tanzania Bara (VPL), straika wa Simba, Ibrahim Ajibu, ametamba kuwa timu yao itatwaa ubingwa msimu huu.

IBRAHIM AJIBU

Timu hiyo ya Msimbazi imeshinda mechi zote sita za VPL ilizocheza tangu kuanza kwa mwaka huu (tano chini ya kocha mpya Mganda Jackson Mayanja) ikifunga magoli 14 huku ikiruhusu nyavu zake kutikiswa mara moja.

Na rekodi hiyo nzuri inampa nguvu straika huyo kusema hadharani kwamba timu yake itamaliza ukame wa miaka minne bila taji la Ligi Kuu msimu huu.

Katika mahojiano na Nipashe mjini hapa jana, Ajibu alisema wamebaini kuwa njia pekee ya kukata kiu ya mataji Msimbazi ni kujituma na kupambana dakika zote za mchezo.

Alisema: “ Si rahisi lakini tutachukua ubingwa msimu huu. Kocha anatupa maelekezo ambayo kwetu yana faida kubwa. Bila shaka na ninazungumza kwa kujiamini kuwa tuna nafasi kubwa ya kutwaa ubingwa na dhamira ya kutwaa ipo.

“Mimi kama straika, nitahakikisha ninatimiza lengo langu la kufunga mabao lakini pia nitashirikiana na wenzangu kuitafutia timu ushindi."

Ajibu amefunga magoli nane katika mechi 18 zilizopita huku ushirikiano wake na straika Mganda Hamis Kiiza ukitengeneza kombinesheni ya hatari Msimbazi.

Habari Kubwa