Ajibu, Yondani kubadili mazoezi

14Nov 2017
Faustine Feliciane
Nipashe
Ajibu, Yondani kubadili mazoezi

BENCHI la ufundi la mabingwa wa soka nchini, Yanga, limepanga kuongeza dozi ya mazoezi mara baada ya kuwasili kwa wachezaji wake waliokuwa kwenye kikosi cha timu ya Taifa 'Taifa Stars'.

Ajibu

Timu hiyo awali ilikuwa ikifanya mazoezi mara moja asubuhi chini ya Kocha Msaidizi, Shadrack Nsajigwa.

Nsajigwa aliliambia Nipashe jana kuwa, wataongeza nguvu ya mazoezi kwa kuwa watakuwa na kikosi kamili na pamoja na Kocha Mkuu, George Lwandamina, ambaye alitarajiwa kurejea nchini jana akitokea kwao, Zambia.

"Hatukuwa na kikosi kamili kwa sababu wengine walikuwa kwenye timu ya Taifa, kureja kwao maana yake hata programu yetu ya mazoezi itabadilika", alisema Nsajigwa.

Alisema mazoezi yao yatalenga kufanya vizuri kwenye mchezo wao ujao dhidi ya Mbeya City.

"Tunafahamu matokeo tofauti zaidi ya ushindi yatatunyon'gonyesha, tunajipanga ili kuhakikisha tunapata ushindi kwenye mchezo ujao," alisema Nsajigwa.

Wachezaji wa Yanga inayodhaminiwa na Kampuni ya Kubashiri Matokeo Michezoni ya SportPesa, waliopo kwenye kikosi cha Stars ni pamoja na Gadiel Michael, Kelvin Yondani, Raphael Daudi pamoja na Ibrahim Ajibu.

Yanga inahaha kuishusha kileleni Simba wanaoongoza ligi kwa tofauti ya pointi mbili ikiwa na pointi 19.

Habari Kubwa