Ali Kiba nd'o 'habari ya mjini' Rwanda

16Mar 2016
Lasteck Alfred
Lete Raha
Ali Kiba nd'o 'habari ya mjini' Rwanda

ALI Kiba ndiye msanii wa Tanzania ambaye ni 'habari ya mjini' kwenye jiji la Kigali na viunga vyake. Nyimbo za msanii huyo; 'Mwana', 'Chekecha Cheketua', 'Lupela', 'Nagharamia', ndizo zinazotamba kwenye kumbi nyingi za starehe nchini Rwanda kuliko msanii mwingine wa Tanzania.

Utafiti uliofanywa na kampuni ya Rosty Entertainment ya jijini Kigali, inaonyeha kuwa Kiba ndiye msanii ambaye nyimbo zake zinapigwa zaidi kuliko wasanii wengine.

Afisa Masoko wa kampuni hiyo, Pierre Bizimana alisema, “Kampuni yetu ya Rosty inahusika na suala zima la muziki. Kwa ufuatiliaji wetu wa kibiashara, msanii wa Tanzania, Ali Kiba, ndiye anayekubalika zaidi nchini Rwanda. Pia Diamond wa Tanzania ni mkali mwingine anayekubalika sana hapa.

“Mbali na hao, pia wapo TMK Wanaume na Ambwene Yesaya 'AY'. Wasanii hao ukiwaalika kwenye shoo unaweza kupata faida kwani ndiyo wanaokubalika zaidi hapa, lakini Kiba ndiye anayeshika rekodi ya kukubali nchini kwetu kwa sasa,” alisema afisa huyo.

Rosty inamiliki kumbi tatu kubwa za starehe, wanaandaa shoo mbalimbali kwa wasanii wa nje, lakini pia ndiyo wanaosimamia baadhi ya wasanii nchini Rwanda.

Wakati Diamond akionekana kuwa maarufu zaidi Afrika huku akiwa na wafuasi wengi kwenye mitandao ya kijamii, hali ni tofauti nchini Rwanda ambako Ali Kiba anafunika zaidi.

Maisha tofauti Rwanda, TZ

Mbali na kutamba kwa wasanii hao, Lete Raha pia ilijaribu kuangalia maisha yalivyo jijini Kigali na hivi ndivyo hali ilivyo. Rwanda na Tanzania zimepisha kwa saa moja. Tanzania iko mbele kwa saa moja. Mfano Tanzania kukiwa saa 2 asubuhi, kule Rwanda ni saa 1 asubuhi.

Hakuna vibanda vya chipsi

Tumezungumzia hili kwasababu chipsi ni moja ya vyakula vinavyotumiwa sana na rika zote. Kwenye majiji kama Dar es Salaam, Mwanza, Dodoma na mengineyo, ulaji wa chipsi unaonekana kuwa mkubwa. Jijini Kigali hakuna vibanda vya chakula, kule watu wanakula kwenye migahawa na majumbani mwao.

Pia unapokuwa kwenye mgahawa au hoteli huwezi kupata chipsi mayai kokote na badala yake unaweza kupata chipsi kavu pekee. Mchanganyo huo wa mayai na chipsi kwao wanauona kama vile ni kitu ambacho hakiwezekani.

Hakuna Machinga

Rwanda si kama Bongo ambako kila mtu anapata uhuru wa kujitafutia riziki hata kwa kusambaza baadhi ya bidhaa zake kwa wanunuzi. Nchini Rwanda suala la wafanyabiashara wadogo maarufu kwa jina la 'Machinga' kuzunguka mtaani ni kinyume cha sheria za nchi hiyo. Wafanyabiashara wote wanatakiwa kuwa ndani ya jengo na kufanya shughuli zao humo humo.

Daladala huduma za Internet bure

Haya ni maendeleo. Nchini Rwanda daladala zao zinatoa huduma za Internet bure kwa wateja wake wote wanaokuwa wakipanda mabasi hayo. Jitihada hizo ni za serikali za kutaka kuona nchi ikiendelea kiteknolojia na mawasiliano.

Daladala kulipia kwa mwezi na si pale unapopanda

Serikali ya Rwanda pia ipo kwenye mchakato wa kubadili utaratibu wa kulipa nauli kwenye daladala nchini humo na kwamba abiria atatakiwa kulipa fedha ya usafiri kwa mwezi mzima kwa mamlaka husika na atapewa risiti ambayo itamwezesha yeye kusafiri na basi lolote na kwa wakati wowote.

Hakuna kusimamisha abiria

Nchini Tanzania, abiria kusimama kwenye usafiri wa daladala ni suala la kawaida, Rwanda ni kinyume cha sheria na mwenye gari na abiria wanaweza kufunguliwa mashataka iwapo watabainika. Pia kusimama kwa daladala sehemu isiyokuwa na kituo ni kosa kubwa na kwamba abiria ukitaka usafiri lazima kwenda kituoni na si kubebewa kokote pale utakapokuwa umesimamisha gari. Hamna mambo ya 'msaada kwenye tuta'.

Ulinzi wa jeshi kila kona

Tanzania tumezoea kuona benki zikilindwa, ofisi kubwa nazo zikilindwa, lakini pia ulinzi umekuwa zaidi kwa ajili ya kazi pale wanapohitajika. Rwanda ni tofauti, askari polisi na jeshi huwa wanatapakaa kila kona ya mji wakilinda amani. Iwapo wewe ni mgeni wa mazingira hayo unaweza kushangaa sana, lakini kiuhalisia ndiyo hivyo.

Hakuna vurugu za bodaboda

Rwanda, waendesha bodaboda ni maarufu kwa jina ‘motor’, huko lazima awe ameandikishwa na anatambulika na serikali, lazima mwendeshaji na abiria wavae kofia ngumu, lakini pia lazima wafuate sheria za usalama barabarani. Nchini Tanzania kumekuwa na tatizo kubwa la waendesha bodaboda kutofuata sheria za usalama barabarani.

Hakuna teksi nyingi

Kila sehemu yenye watu wengi kwenye majiji ya Tanzania ni lazima ukute huduma za teksi, Rwanda ni tofauti. Kwenye viwanja vya ndege tu ndipo unapoweza kupata teksi, sehemu zingine usafiri wa bodaboda unatawala.

Hakuna waokota chupa za plastiki

Nchi ya Rwanda imedhibiti matumizi ya plastiki. Unapoenda kununua chupa ya maji ya lita tano lazima urudishe chupa ya maji ambayo ulishaitumia vinginevyo utalazimika kununua chupa hiyo ya plastiki kwa kiasi cha Sh. 2,000 ya Tanzania.

Hakuna nazi

Kila ukizunguka kwenye maduka ya vyakula, huwezi kukuta nazi. Watu wengi hawafahamu nazi ilivyo zaidi ya kuisoma kwenye vitabu. Kila unapoenda migahawani huwezi kukuta chakula kilichowekwa nazi. Nazi ni maarufu nchini Tanzania na hutumiwa kuongeza ladha kwenye chakula.

Thamani ya pesa yao ipo juu
Pesa ya Tanzania haina thamani kubwa kama ile ya Rwanda, mfano unapokuwa na Sh.1,500 za Kitanzania ni sawa na Faranga 500 tu za Rwanda.

Warembo

Hakika kila nchi inatambulika kwa vitu vizuri na watu waliopo, Tanzania tunaaminika kwa kuwa na vivutio vizuri na madini lakini Rwanda kuna wanawake warembo na wanaume wazuri na wenye mvuto ambao wana muonekano wa kitofauti na wale wanaopatikana Tanzania.

Urembo walionao vimwana wa Rwanda umekuwa mijadala inayofanyiwa utani sana katika mitandao ya kijamii. Mfano kuelekea mechi ya Yanga dhidi ta APR, picha ya vimwana warembo wanaoonekana wakiingia uwanjani ilizua utani kuwa ndiyo 'cheerleaders' au waokota mipira wa mechi hiyo.

Vijana wagumu kuoa

Kwa kuhofia kufilisiwa mali kutokana na sheria iliyoweka na nchi, imefanya vijana wengi wasioe na badala yake wengi wanaishia kuwa na uhusiano tu. Hali hiyo inatokana na kile kilichopitishwa kisheria kuwa endapo ndoa inavunjika, mali zinagawanywa nusu kwa nusu.

Mpangilio mzuri wa jiji

Kuna mifereji iliyopangiliwa vizuri na iliyotengenezwa kwa uimara wa hali ya juu. Inapotokea kuna mvua, ni ngumu kuona ikiziba au hata ikiharibika kutokana na jinsi walivyopanga mambo.

Habari Kubwa