Alliance yahofia Biashara kuihujumu

14May 2019
Na Mwandishi Wetu
Nipashe
Alliance yahofia Biashara kuihujumu

WAKATI Ligi Kuu Tanzania Bara ikiwa inaelekea ukingoni, uongozi wa Alliance FC umeitaka Bodi ya Ligi kuhakikisha mechi yao dhidi ya Biashara United United itakayochezwa leo kwenye Uwanja wa Karume mjini Musoma inaonyeshwa mubashara.

Biashara United ambao ni wenyeji na wamecheza mechi 34 wana pointi 40 na Alliance FC kutoka jijini Mwanza wao wana pointi 41, lakini wameshuka dimbani mara 35.

Akizungumza na gazeti hili jana, Mwenyekiti wa Kamati ya Mashindano ya Alliance FC, Yusufu Budodi, alisema wameomba mchezo huo urushwe hewani mubashara kwa sababu wanaamini itasaidia kupunguza vitendo vya uonevu ambavyo vimekuwa vikijitokeza katika uwanja huo.

Budodi alisema wanaifahamu vema Biashara United na wangependa kuona timu inayostahili inapata pointi zake kihalali katika mechi hiyo.

"Tunajuana vema, pale Musoma pamekuwa na historia ya vurugu, ni vizuri mchezo wetu ukaonyeshwa "live", hii itawafanya wale wenye nia mbaya wakaacha kwa sababu watajua wataonekana," alisema kiongozi huyo.

Afisa Mtendaji Mkuu wa Bodi ya Ligi, Boniface Wambura, alisema ofisi yake haijapokea barua yoyote kutoka kwa Alliance FC, lakini inafanya kazi kwa weledi kuhakikisha mechi zote zinachezeshwa kwa haki.

Wambura alisema kuwa bodi inatuma wasimamizi mbalimbali wanaojulikana na wasiojulikana katika mechi zote zilizobaki na kuwaondoa hofu wadau ambao wana wasiwasi na hali ya upangaji matokeo.

Ligi Kuu Tanzania Bara msimu wa 2018/19, inatarajiwa kumalizika ifikapo Mei 28, mwaka huu na msimu huu utafungwa kwa mchezo wa fainali ya mashindano ya Kombe la FA utakaochezwa Juni Mosi kwenye Uwanja wa Ilulu, Lindi kwa kuwakutanisha Azam FC na Lipuli FC.

Habari Kubwa