Amunike aichambua Stars kipigo Senegal

25Jun 2019
Somoe Ng'itu
CAIRO
Nipashe
Amunike aichambua Stars kipigo Senegal
  • ***Asema bado wananafasi Afcon,  Nyoni sasa fiti kuivaa Harambee Stars Alhamisi, kazi kwa kocha...

 LICHA ya kuanza vibaya fainali za Kombe la Mataifa ya Afrika (Afcon) 2019, Kocha Mkuu wa Timu ya Tanzania (Taifa Stars), Mnigeria Emmanuel Amunike, amesema bado anakiamini kikosi chake kinachoshiriki mashindano hayo baada ya kuikosa michuano hiyo kwa miaka 39.

Kocha Mkuu wa Timu ya Tanzania (Taifa Stars), Mnigeria Emmanuel Amunike.

Taifa Stars ilipoteza mechi yake ya kwanza ya Kundi C kwa kufungwa mabao 2-0 na Senegal ambayo ilitumia wachezaji wote wanaocheza soka la kulipwa barani Ulaya.

Amunike aliliambia gazeti hili kuwa mchezo dhidi ya Senegal ulikuwa ni mgumu kwa timu yake, lakini anawapongeza wachezaji wake kwa namna walivyopambana kuhakikisha wanawabana vigogo hao kutoka Afrika Magharibi.

Alisema hata wapinzani wao pia walipata tabu katika kufanya mashambulizi katika mchezo huo, na changamoto hiyo iliwafanya wabadilishe mfumo kila wakati ili kuwafanya Senegal washindwe kutawala mchezo kwa kipindi kikubwa.

"Mechi ilikuwa ngumu, na hata kwao pia, naamini watakuwa wanasema wamekutana na timu tofauti na ile ambayo waliifikiria kabla ya mchezo kuanza, wachezaji wangu wanaendelea kujifunza mbinu, kutokana na kila wanachokiona baada ya kumaliza mchezo mmoja," alisema Amunike.

Kocha huyo aliongeza kuwa bado nafasi ya kusonga mbele katika mashindano hayo ipo, kwa sababu kila timu imebakiza michezo miwili ya hatua hiyo ya makundi ambayo itamalizika Julai Mosi.

"Wachezaji wangu wanasonga mbele, ugumu na changamoto wanazokutana nazo, huwasaidia kuwajenga, wanaimarika na nina matumaini watafanya vema mchezo wa pili dhidi ya Kenya, najua wanajuana lakini sasa wanakutana katika mashindano ya ngazi ya juu Afrika," Amunike aliongeza.

Naye beki wa pembeni wa Stars, Hassan Kessy, alisema kuwa makosa mawili waliyofanya ndiyo yaliwapa wapinzani wao Senegal nafasi za kufunga katika mchezo huo.

Hata hivyo beki huyo wa zamani wa Mtibwa Sugar, Simba na Yanga alisema kwamba watarekebisha makosa hayo na kuingia wakiwa makini zaidi katika mchezo dhidi ya Harambee Stars ya Kenya ili wapate ushindi na kuweka matumaini ya kusonga mbele kwenye fainali hizi zinazofanyika kwa mara ya 13.

NYONI AREJEA

Katika hatua nyingine beki wa kati mkongwe wa Taifa Stars, Erasto Nyoni, amesema kuwa afya yake imeimarika na anaamini atakuwa tayari kucheza mechi ya pili ya Kundi C ya Harambee Stars keshokutwa.

Nyoni alikosa mchezo wa kwanza wa fainali hizo dhidi ya Senegal, ambapo Taifa Stars ilifungwa mabao 2-0, kutokana na maumivu ya nyama za paja.

Beki huyo kiraka alipata maumivu hayo katika mechi ya kirafiki ya kimataifa dhidi ya Misri iliyochezwa Juni 13, mwaka huu, ambayo pia ilimpa majeraha ya goti, beki mwingine wa timu hiyo, Aggrey Moris ambaye anasubiri kufanyiwa upasuaji nchini Afrika Kusini.

Akizungumza na gazeti hili jana, Nyoni, alisema kwa sasa afya yake imeimarika na ameanza mazoezi ya pamoja na wachezaji wenzake kwa kushiriki programu zote zinazotolewa na benchi la ufundi.

"Nimepona, msiwe na wasiwasi, mechi ijayo nitacheza, labda kocha aamue vingine," alisema kwa kifupi beki huyo wa zamani wa mabingwa wa Kombe la FA, Azam FC ya jijini Dar es Salaam.

Habari Kubwa