Amunike atoa msimamo Stars

05Jul 2019
Shufaa Lyimo
Dar es Salaam
Nipashe
Amunike atoa msimamo Stars

KOCHA Mkuu wa Timu ya Taifa ya Tanzania (Taifa Stars), Emmanuel Amunike, amesema matokeo waliyoyapata Cairo Misri kwenye fainali za Kombe la Mataifa ya Afrika (Afcon) 2019, wamejifunza mengi licha ya kupata vipigo katika mechi zote tatu za hatua ya makundi.

Emmanuel Amunike.

Akizungumza na waandishi wa habari jana  mchana mara baada ya kuwasili katika Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Julius Nyerere, alisema hajawafurahisha mashabiki na Watanzania kwa ujumla kutokana na matokeo hayo, lakini sasa anaelekeza nguvu zake katika mashindano ya kuwania kufuzu fainali za Wachezaji wanaocheza Ligi za Ndani (CHAN) ambazo fainali zake zitafanyika mwakani nchini Cameroon.

“Naamini wachezaji wamejifunza mambo mengi Afcon kwa sababu wamekutana na timu zenye viwango vya juu, hivyo tutaanza maandalizi kwa ajili ya CHAN,” alisema Amunike kwa kifupi huku akieleza kikosi kitakachoivaa Sudan kuelekea kuwania kufuzu CHAN atakiweka bayana baadaye.

Kwa upande wake Waziri mwenye dhamana ya michezo Harrison Mwakyembe, alisema kuwa wachezaji wamejitahidi kwa hatua waliyofikia na kudai baada ya miaka miwili Tanzania ina uhakika wa kushiriki kwa mara nyingine michuano kama hiyo.

Aidha, aliwataka Watanzania na wadau wa soka hapa nchini kuacha kuwazodoa wachezaji kwa matokeo waliyoyapata na badala yake waendelee kuisapoti timu hiyo ili iweze kufanya vizuri kwenye mashindano yaliyopo mbele yao.

Naye Mwenyekiti wa Kamati ya Uhamasishaji wa timu hiyo, Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Paul Makonda, aliewataka Watanzania waendelee kuiunga mkono timu yao kama walivyokuwa wamewafanyia katika kipindi kile ilipofuzu fainali za Afcon.

“Taifa Stars imeanza vizuri nina imani walichokifanya wachezaji wetu kitaendelea kuwa bora zaidi kwani wameonyesha juhudi ya hali ya juu,” alisema Makonda.