Amunike: Zamu ya Taifa Stars Afcon

21Mar 2019
Na Mwandishi Wetu
Dar es Salaam
Nipashe
Amunike: Zamu ya Taifa Stars Afcon

NI zamu yetu! Kocha Mkuu wa Timu ya Soka ya Taifa (Taifa Stars), Emmanuel Amunike, amesema Tanzania inastahili na ina nafasi ya kufuzu kucheza fainali zijazo za Kombe la Afrika (Afcon 2019) Juni nchini Misri.

Taifa Stars inatarajia kuikaribisha Uganda (Cranes) katika mchezo wa mwisho utakaochezwa Jumapili kwenye Uwanja wa Taifa jijini Dar es Salaam na inahitaji matokeo ya ushindi tu ili iweze kufuzu fainali hizo.

Akizungumza jana jijini, Amunike alisema ni ukweli kuwa wapinzani wao Uganda ni wazuri, lakini Taifa Stars pia ni wazuri, hivyo anaamini kikosi chake kitaibuka na ushindi katika mchezo huo wa Jumapili na kutimiza ndoto ya muda mrefu ya Watanzania kushiriki fainali hizo.

Amunike alisema anafahamu vema kuwa Uganda wanataka kuona wanaendeleza rekodi yao ya kupata ushindi, lakini bidii na kiwango ambacho Stars imepanga kuonyesha kwenye uwanja wa nyumbani vinampa nguvu ya kuamini hakuna kitakachowakwamisha.

"Hakuna ambaye aliamini tunaweza kuondoka na pointi Kampala, lakini tulifanikiwa kupata, sasa tunacheza nyumbani kwetu, mbele ya familia zetu, mbele ya wake zetu, mbele ya kaka zetu, mbele ya baba zetu, mbele ya dada zetu, nafikiri tunatakiwa kujiamini kuwa tutatimiza ndoto zetu, tukijituma, nina uhakika tutafuzu," alisema Amunike.

Mnigeria huyo aliongeza kuwa anafurahi kuona wachezaji wote aliowaita wako 'fiti, na wamefanya mazoezi kwa siku mbili na kila mmoja morali yake iko juu kuhakikisha wanatekeleza jukumu ambalo Watanzania wanalisubiri.

"Kuna wachezaji ambao walikuwapo mechi zilizopita na wengine ni wapya, hii ni moja ya mchakato wa maendeleo, tunayafanyia kazi makosa ambayo yalijitokeza katika michezo iliyopita ili yasijirudie, kwa sababu tunajua tukishinda Jumapili tutakuwa tumefuzu," Amunike alisema.

Aliongeza kuwa Uganda ina kikosi kizuri, lakini yeye amejipanga kuwavaa tofauti na wanavyoifahamu Stars kwa sababu kila mechi ina mipango yake tofauti.

"Najua Uganda ni wazuri, wako makini lakini nina hakika tutawadhibiti, hatuna hofu yoyote dhidi yao," aliongeza kocha huyo kabla ya kuanza mazoezi ya jioni kwenye Uwanja wa Taifa.

Habari Kubwa