Aussems aanika kikosi  cha kuwaua Waarabu 

10Jan 2019
Isaac Kijoti
Zanzibar
Nipashe
Aussems aanika kikosi  cha kuwaua Waarabu 
  • *** Chama, Okwi, Kagere kuongoza ushambuliaji, Kwasi, Coulibaly waachwa chini ya Mgosi...

HATIMAYE kikosi kitakachokuwa na jukumu la kuhakikisha Simba inaanza Ligi ya Mabingwa Afrika hatua ya makundi kwa kuibuka na pointi tatu muhimu, kimeanikwa rasmi.

Simba iliyokuwa na jeshi lake kamili la wachezaji 27, visiwani hapa kwa ajili ya Kombe la Mapinduzi, itaialika JS Saoura ya Algeria Jumamosi katika mechi ya Ligi ya Mabingwa itakayopigwa Uwanja wa Taifa jijini Dar es Salaam.

Katika michuano ya Kombe la Mapinduzi, Simba imetinga nusu fainali kwa kushinda mechi zote tatu, hivyo Kocha Mkuu, Patrick Aussems, akachukua jukumu la kukigawa kikosi chake na nusu kurejea nacho jijini Dar es Salaam tayari kwa mechi hiyo ya Ligi ya Mabingwa dhidi ya Waarabu hao wa Algeria.

Akizungumzia michuano hiyo baada ya ushindi wa juzi wa bao 1-0 dhidi ya Mlandege, Aussems alisema kazi iliyobaki sasa ni ya kikosi B ambacho kitaungana na baadhi ya nyota wachache wa kikosi cha kwanza.

Nipashe jana iliwashuhudia wachezaji 18 watakounda kikosi cha kwanza kuivaa JS Saoura, wakiondoka visiwani hapa kurudi Dar es Salaam kwa ajili ya mechi hiyo, ambao ni Aishi Manula, Shiza Kichuya, Meddie Kagere, John Bocco, Nicholas Gyan, Pascal Wawa, Clatious Chama, Emmanuel Okwi na Haruna Niyonzima.

Wengine waliopata nafasi hiyo ya kuchaguliwa na Aussems ni James Kotei, Deogratius Munishi 'Dida', Hassan Dilunga, Juuko Murshid, Rashid Juma, Mohemmed Hussen 'Tshabalala', Mzamiru Yassin, Said Ndemla na Jonas Mkude.

Nyota wengine waliobaki Aussems alisema wataungana na baadhi ya Kikosi B cha Simba ambacho kiliwasili visiwani hapa jana mchana kwa ajili ya kuendelea na michuano hiyo ya Kombe la Mapinduzi.

Wachezaji waliobaki visiwani hapa ni Asante Kwasi, Yusuf Mlipili, Adam Salamba, Ally Salim, Zana Coulibaly, Abdul Seleman, Mohamed Ibrahim (MO) na Paul Bukaba.

Kikosi hicho kitakuwa chini ya kocha Niko Kiondo akisaidiwa na Mussa Hassan Mgosi.

Katika michuano ya Kombe la Mapinduzi inayoendelea kwenye Uwanja wa Amaan visiwani hapa, Simba ilianza kwa kushinda 4-1 dhidi ya Chipukizi ya Pemba, kisha kuichapa KMKM bao 1-0 na juzi kuhitimisha hatua ya makundi kwa ushindi wa bao 1-0 dhidi ya Mlandege.

Bao hilo dhidi ya Mlandege lilifungwa na Harouna Niyonzima kwa mkwaju wa penalti dakika ya 21 kufuatia Asante Kwasi kuchezewa madhambi ndani ya 18.

Habari Kubwa