Aussems afunguka anapoihofia Mtibwa

16May 2019
Somoe Ng'itu
DAR ES SALAAM
Nipashe
Aussems afunguka anapoihofia Mtibwa
  • ***Asema ushindi unaweza kupatikana, awaonya wachezaji Simba kuwa watapaswa...

BAADA ya kupunguzwa kasi katika mbio za ubingwa kwenye michezo miwili iliyopita, mabingwa watetezi, Simba, wanarejea dimbani kuwakaribisha Mtibwa Sugar katika mechi ya Ligi Kuu Tanzania Bara itakayochezwa leo kwenye Uwanja wa Uhuru jijini Dar es Salaam.

Kocha Mkuu wa Simba, Mbelgiji Patrick Aussems.

Mechi hiyo ni ya kiporo na timu hizo mbili zitakutana tena katika mchezo wa kufunga pazia msimu huu wa 2018/19 ambao utachezwa Mei 28, mwaka huu kwenye Uwanja wa Jamhuri mkoani Morogoro.

Akizungumza na Nipashe jana, Kocha Mkuu wa Simba, Mbelgiji Patrick Aussems, aliliambia gazeti hili kuwa anatarajia kukutana na ushindani katika mchezo huo, kwa sababu wapinzani wao hawana presha ya aina yoyote.

Aussems alisema kuwa amewataka wachezaji wake kusahau matokeo ya mechi ziliyopita, na kuangalia mchezo dhidi ya Mtibwa Sugar ambao upo mbele yao.

"Itakuwa mechi ngumu, Mtibwa Sugar ni wazuri, wana wachezaji wenye uwezo na wazoefu, lakini tunatarajia tutapata matokeo mazuri," alisema Mbelgiji huyo.

Naye Meneja wa Simba, Patrick Rweyemamu, alisema wamejiandaa kupambana na kuonyesha kiwango cha juu kama ilivyokuwa katika mchezo uliopita.

Rweyemamu alisema wachezaji wote wako tayari kwa mchezo huo na wanajua bidii pekee ndiyo itakayowasaidia kutimiza malengo yao.

"Tutaenda kupambana, kama tulivyopambana katika mechi ya Azam, ari ya wachezaji ilikuwa juu sana, kwa kifupi nikwambie wachezaji wote wako tayari, isipokuwa Wawa (Paschal), ila naamini tutakuwa naye katika mechi za mbele ya safari," Rweyemamu alisema.

Yanga ambao wamecheza mechi 36 na wana pointi 83, ndio vinara wa ligi hiyo yenye kushirikisha timu 20 ikifuatiwa na Simba yenye pointi 82 zilizotokana na mechi 33 wakati mabingwa wa Kombe la Kagame, Azam FC wanafuatia wakiwa na pointi 69 baada ya kushuka dimbani idadi sawa ya michezo na Wanajangwani hao.