Aussems akubali Prisons wanajua

09Nov 2019
Somoe Ng'itu
Dar es Salaam
Nipashe
Aussems akubali Prisons wanajua

BAADA ya timu yake kushindwa kutamba, Kocha Mkuu wa Simba, Patrick Aussems, amesema kuwa kikosi cha Tanzania Prisons ni imara na kimempa ushindani wa hali ya juu katika mchezo wa Ligi Kuu Bara uliowakutanisha kwenye Uwanja wa Uhuru jijini Dar es Salaam juzi.

Akizungumza na gazeti hili, Aussems, alikisifia kikosi cha Prisons kwa kuonyesha soka safi na kwamba ni mara yake ya kwanza kukutana na timu iliyojipanga vema.

Aussems alisema kuwa wapinzani wao walifanikiwa kuwabana na hivyo, nyota wake walishindwa kufanya mashambulizi kila walivyokuwa wanajipanga kuelekea kwenye lao la Prisons, hali iliyopelekea mchezo huo kumalizika kwa sare ya bila kufungana.

Alisema pia hakushangazwa na kiwango na Prisons, kwa sababu ndiyo timu pekee ambayo haijapoteza mchezo hata mmoja tangu msimu huu ulipoanza.

"Tangu nimekuja Tanzania, hii ni mara ya kwanza kuona timu iliyojipanga kama hii, walikuja hapa kwa ajili ya kupunguza nafasi, walikuja kwa lengo la kujilinda, walijilinda vizuri, nawapongeza kwa hilo," alisema Aussems.

Naye nahodha msaidizi wa Simba, Erasto Nyoni, alisema kuwa mechi hiyo ilikuwa na ushindani na siku hiyo ya juzi, timu yao haikuwa na bahati.

"Ilikuwa ni mechi ngumu, kwetu na kwao pia, tuliingia na mbinu zetu, lakini tulishindwa kupenya, tulipambana, tulitumia njia mbalimbali kuhakikisha tunafika golini, lakini hatukuweza kupata bao," alisema beki huyo.

Baada ya kumalizika kwa majukumu ya Timu ya Taifa (Taifa Stars), ambayo inakabiliwa na mechi mbili za kuwania tiketi ya kushiriki fainali za Kombe la Mataifa ya Afrika (Afcon 2021), Simba itakutana na Ruvu Shooting katika mechi nyingine ya Ligi Kuu Bara itakayochezwa Novemba 24, mwaka huu kwenye Uwanja wa Uhuru jijini.

Mabingwa hao watetezi, Simba ambao wamecheza mechi tisa ndio vinara wa ligi hiyo wakiwa na pointi 22, wakati Singida United yenye pointi nne lakini imeshuka dimbani mara 10, inaburuza mkia.

Habari Kubwa