Aussems azisoma mbinu za Waarabu

07Jan 2019
Isaac Kijoti
Zanzibar
Nipashe
Aussems azisoma mbinu za Waarabu
  • Atumia Mapinduzi Cup kuisuka Simba ili kufanya mauaji Taifa Jumamosi, asema tayari...

LICHA ya kikosi chake kuonekana kimekamilika kimbinu kwenye michuano ya Kombe la Mapinduzi, Kocha Mkuu wa Simba, Patrick Aussems, amesema kuna mambo anayafanyia kazi kuelekea mechi dhidi ya JS Saoura itakayochezwa Jumamosi kwenye Uwanja wa Taifa jijini Dar es Salaam.

Kocha Mkuu wa Simba, Patrick Aussems

Jana usiku Simba ilishuka tena kwenye Uwanja wa Amaan visiwani hapo kuivaa KMKM ikiwa ni baada ya kuichapa Chipukizi ya Pemba kwa mabao 4-1 katika mechi yao ya kwanza ya michuano ya Kombe la Mapinduzi mwaka huu.

Akizungumza na Nipashe, Aussems alisema kwa kupitia mikanda ya video tayari ameshaona namna JS Saoura inavyocheza, na katika kila mechi wanayocheza anafanyia kazi jinsi ya kuivaa miamba hiyo ya Algeria.

"Katika mazoezi na hizi mechi za Mapinduzi nitakuwa nakiandaa kikosi changu namna nzuri ya kuwavaa JS Saoura, huko ndiko akili yangu ilipo kwa sasa.

"Na baada ya mechi yetu ya tatu (dhidi ya Mlandege kesho), tutarudi Dar es Salaam kwa maandalizi zaidi, malengo yetu yapo Ligi ya Mabingwa si Mapinduzi Cup," kocha huyo raia wa Ubelgiji alisema.

"Sina wasiwasi, natumai tutafanya vizuri pia katika michuano hii, ila itabidi turejee Dar es Salaam na kikosi cha pili kitakuja kumalizia tulipoishia."

Aussems ambaye amekuwa akipongezwa na mashabiki wa Simba visiwani hapa kwa kushusha kikosi kamili cha timu hiyo kwenye michuano hiyo, alisema ataendelea kuwachezesha wachezaji wake wote.

Alisema lengo lake ni kuwaandaa kwa mechi hiyo ya Ligi ya Mabingwa Afrika, hivyo hiyo ni fursa kwake ya kukiandaa kikosi chake kwa mapana zaidi.

Wakati Simba ikishinda 4-1 dhidi ya Chipukizi, JS Saoura ilichezea kichapo cha bao 1-0 nyumbani katika Uwanja wao wa Stade 20 Aout 1955 kwenye mechi ya Ligi Kuu Algeria maarufu Ligue 1, dhidi ya JS Kabylie.

Kadhalika, wakati Simba ikiivaa Mlandege kesho, JS Saoura itakuwa ugenini dhidi ya MC Oran kwenye mechi yao ya pili tangu kuanza kwa mzunguko wa pili wa ligi hiyo inayoshirikisha timu 16.

Baada ya mchezo huo, JS Saoura itapanda pipa kuifuata Simba katika mechi hiyo ya kwanza ya hatua ya makundi ya michuano hiyo yenye utajiri mkubwa kwa ngazi ya klabu inayoandaliwa na Shirikisho la Soka Afrika, Caf.