Aussems: Hatutapaki basi Kongo

16Jan 2019
Na Mwandishi Wetu
Dar es Salaam
Nipashe
Aussems: Hatutapaki basi Kongo

WAKATI kikosi cha Simba kinatarajiwa kuondoka kesho kwenda Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo kwa ajili ya mchezo wao wa pili hatua ya makundi ya Ligi ya Mabingwa Afrika dhidi ya AS Vita, Kocha Patrick Aussems, amesema kamwe hawatacheza soka la kujilinda kwenye mchezo huo.

Akizungumza na gazeti hili jana baada ya mazoezi yaliyofanyika kwenye uwanja wa Boko Veteran, Aussems, alisema kuwa wanawaheshimu wapinzani wao kwa kuwa ni moja ya timu nzuri na kubwa Afrika.

“Tuna kikosi kizuri na sisi, ukitazama namna tulivyocheza mchezo uliopita utaona tunaweza kucheza soka letu na kulazimisha matokeo mazuri, hatutacheza soka la kujilinda muda wote,” alisema Aussems.

Alisema kuwa leo watafanya mazoezi ya mwishoasubuhi kabla ya kesho kuanza safari ya kuwafuata AS Vita.

Wakati Simba wakiibuka na ushindi wa mabao 3-0 kwenye mchezo wao wa kwanza dhidi ya JS Saoura Jumamosi iliyopita kwenye uwanja wa Taifa, AS Vita wenyewe walikumbana na kipigo cha mabao 2-0 kutoka kwa Al Ahly ya Misr.

Wakati huo huo, kiungo wa Simba, Said Ndemla, leo anaanza majaribio yake kwenye klabu ya Eskilstuna baada ya kuwasili salama juzi.

Ndemla kama atafuzu majaribio atasajiliwa na klabu hiyo inayoshiriki ligi kuu ya Sweden.

Habari Kubwa