Aussems: Hesabu sasa kwa Mtibwa

15May 2019
Somoe Ng'itu
DAR ES SALAAM
Nipashe
Aussems: Hesabu sasa kwa Mtibwa

TUTAZINDUKA! Kocha Mkuu wa Simba, Patrick Aussems, amesema alijiua mapema kabla ya mchezo dhidi ya Azam FC kama atapoteza pointi kutokana na aina ya mfumo ambao wapinzani hao walikuwa wakicheza katika mechi hiyo ya Ligi Kuu Tanzania Bara ambayo ilimalizika kwa sare ya bila kufungana.

Kocha Mkuu wa Simba, Patrick Aussems.

Hata hivyo, Aussems alisema anaamini timu yake itarejea katika kasi yake ya ushindi katika mechi zinazofuata ambazo ni dhidi ya Mtibwa Sugar ya Turiani, Morogoro itakayochezwa kesho na Ndanda FC kutoka Mtwara ambayo watavaana ifikapo Mei 19, mwaka huu, zote kwenye Uwanja wa Uhuru jijini Dar es Salaam.

Aussems alisema wachezaji wake walifanya kila linalowezekana kuhakikisha wanafunga bao katika mechi hiyo dhidi ya Azam, lakini hali ilikuwa ngumu kwa sababu mabingwa hao wa Kombe la Kagame waliingia kwa dhamira moja ya kujilinda.

"Tulijaribu kutumia krosi, kucheza pasi za chini, kupiga mipira mirefu, lakini hatukufanikiwa, pia tulijaribu kucheza kupitia upande wa kulia, kushoto na katikati, lakini pia tulishindwa kufanikiwa, na unapogundua huwezi kupata ushindi, unajitahidi usipoteze pointi," alisema Aussems.

Mbelgiji huyo alisema anawapongeza wachezaji wake kwa kutokata tamaa ya kusaka ushindi kwa sababu wanajua bado malengo yao ya kutetea taji hilo hayajatimia.

"Tutajipanga vizuri katika mechi nyingine zinazofuata, Alhamisi tutacheza dhidi ya Mtibwa Sugar, halafu Ndanda, ingawa tunajiandaa kukutana na ushindani pia," aliongeza kocha huyo anayesaidiwa na Dennis Kitambi.

Mechi nyingine za Simba zilizosalia msimu huu ni dhidi ya Singida United (ugenini), Biashara United (Uhuru) halafu itasafiri kuwafuata Mtibwa Sugar katika mchezo wa marudiano ambao utafunga pazia la msimu wakati huu ikiwa na pointi 82, na  ikihitaji pointi tisa ili iweze kutetea ubingwa.

Habari Kubwa