Aussems, kocha Nkana wategana

07Dec 2018
Somoe Ng'itu
Dar es Salaam
Nipashe
Aussems, kocha Nkana wategana
  • ***Chama, Kessy watajwa kuelekea mchezo huo wa raundi ya kwanza...

KIKOSI cha Simba kilirejea nchini jana mchana, huku kocha wake Mbelgiji, Patrick Aussems, akisema watajipanga imara kuhakikisha wanapata matokeo mazuri katika mechi zao zote mbili za raundi ya kwanza kwenye mashindano ya Ligi ya Mabingwa Afrika dhidi ya Nkana FC ya Zambia.

kocha wa simba Mbelgiji, Patrick Aussems

Aussems ambaye timu yake itaanzia ugenini kati ya Desemba 14 na 16 mwaka huu, aliliambia gazeti hili jana, kuwa hakuna mechi rahisi katika mashindano yoyote duniani, kikubwa ni wachezaji kupambana kusaka ushindi.

"Tutacheza na Nkana, ni timu nzuri, imekuwa na matokeo mazuri katika mashindano ya Afrika hivi karibuni, pia sisi tumejipanga kufanya vizuri mwaka huu, malengo yetu kwanza ni kufika hatua ya makundi," alisema kocha huyo.

Naye Kocha wa Nkana FC, Beston Chambeshi, amewapa wapinzani wake, Simba ya jijini Dar es Salaam asilimia 50 na timu yake kiasi kama hicho katika mechi watakayokutana ya raundi ya kwanza ya mashindano ya Ligi ya Mabingwa Afrika.

Chambeshi alisema hayo juzi baada ya kuwaondoa UD Songo katika hatua ya awali ya mashindano hayo kwa kuwafunga jumla ya mabao 3-1.

"Itazame Simba. Nafikiri nao pia wanaizungumzia Nkana. Kwa hiyo ni mchezo ambao kila upande una asilimia 50/50. Wana mchezaji Mzambia kwenye timu yao na sisi pia tuna mchezaji Mtanzania kwenye timu yetu. Kila upande unahitaji kujiandaa vyema kwa ajili ya mchezo huo," alisema Chambeshi katika mahojiano na gazeti la Observer la Zambia.

Nkana iliwafunga mabingwa hao wa Ligi Kuu Msumbuji, UD Songo nyumbani na ugenini na kusonga mbele kwenye michuano hiyo ya kimataifa inayofanyika kila mwaka chini ya usimamizi wa CAF.

Simba, ambao ni mabingwa watetezi wa Ligi Kuu Tanzania Bara pia iliwafunga wapinzani wao Mbabane Swallows ya Swaziland nyumbani na ugenini na kufanya kichapo kuwa cha jumla ya mabao 8-1.

Mchezaji Mzambia ambaye yuko Simba ni kiungo aliye kwenye kiwango cha juu, Clatous Chama, wakati beki wa zamani wa Simba na Yanga, Hassan Kessy, ndiye Mtanzania anayecheza soka la kulipwa katika klabu hiyo yenye makao yake mjini Kitwe.

Habari Kubwa