Aussems: Muda ndio utaongea vs Al Ahly

11Feb 2019
Somoe Ng'itu
Dar es Salaam
Nipashe
Aussems: Muda ndio utaongea vs Al Ahly
  • ***Wakati Wamisri hao wakitua na kujifua Gymkhana, MO naye awaita mashabiki Taifa huku akisema...

WAKATI kikosi cha mabingwa wa zamani wa Afrika, Al Ahly kikiwa kimeshawasili nchini tangu jana asubuhi, Kocha Mkuu wa Simba, Mbelgiji Patrick Aussems, amesema ameshakamilisha programu kwa ajili ya kuwavaa Waarabu hao kutoka Misri.

Kocha Mkuu wa Simba, Mbelgiji Patrick Aussems, picha mtandao

Simba inatarajia kuwakaribisha Al Ahly kesho katika mechi ya raundi ya nne ya hatua ya makundi itakayochezwa kesho kwenye Uwanja wa Taifa jijini Dar es Salaam.

Akizungumza na gazeti hili jana, Aussems alisema kikosi chake kimeimarika na hali hiyo imetokana na mafunzo waliyopata baada ya kupoteza mechi mbili mfululizo za mashindano hayo ya kimataifa.

Aussems alisema amefanya kazi ya kuwanoa nyota wake kwa kuchambua kila kosa lililotokea na kujihami na yanayoweza kutokea katika mchezo wa kesho ambao utachezwa kuanzia saa 10:00 jioni.

Kocha huyo alisema anatarajia kuona wapinzani wao wakicheza tofauti na walivyoonekana katika mechi ya kwanza huku wakijua ubora wa kila mchezaji baada ya kukutana nao.

Alisema licha ya wapinzani wao kupata ushindi katika mechi ya kwanza wakiwa nyumbani kwao, anafahamu hawataingia uwanjani wakibweteka na matokeo yaliyopita na hapo ndio ushindani utakapoanzia.

"Tunasubiri muda, tumeshamaliza mazoezi kuelekea mchezo huo, utakuwa mgumu kwa kila upande, kila timu itaingia uwanjani ikiwa na malengo yake, kwetu ni zaidi ya fainali, tunataka kurejea katika ushindani," alisema kocha huyo.

Naye Mwenyekiti wa Bodi ya Kampuni ya Simba, Mohamed "MO" Dewji alisema jana kuwa wanachama na mashabiki wa klabu hiyo wasiogope kwa sababu hakuna timu ya mpira ambayo haijawahi kufungwa.

"Hakuna ambaye hajawahi kushindwa, kikubwa ni kujipanga upya na kusonga mbele," alisema Dewji ambaye Kampuni yake ya Mohamed Enterprises (METL) ilikuwa ikiidhamini Simba mwaka 2003 ilipotinga hatua ya robo fainali ya michuano hiyo.

Baada ya mechi ya kesho, mabingwa hao watetezi wa Ligi Kuu Tanzania Bara wataendelea kujifua kuwasubiri watani zao, Yanga watakapokutana katika mechi ya Ligi hiyo itakayochezwa Jumamosi kwenye Uwanja wa Taifa.

Aidha, Kikosi cha timu ya Al Ahly kilitua usiku wa kuamkia jana, na jana jioni kilitarajia kufanya mazoezi kwenye Uwanja wa Gymkhana.

Habari Kubwa