Aussems: Simba anzeni sherehe

21May 2019
Somoe Ng'itu
DAR
Nipashe
Aussems: Simba anzeni sherehe
  • ***Rekodi ya kubebea ubingwa Singida yanukia kujirudia leo, awataka mashabiki kuufanya...

HESABU zitatimia? Wakati swali hilo likitikisa kichwani kwa mashabiki wa Simba kuelekea mechi yao ya leo ugenini dhidi ya Singida United, Kocha Mkuu wa 'Wekundu wa Msimbazi' hao, Mbelgiji Patrick Aussems,-

Patrick Aussems.

amewataka kujiandaa kuufanya mji wa Singida kuwa maalum kwao kwa ajili ya kusherehekea ubingwa wa Ligi Kuu 2018/19.

Katika mechi hiyo itakayochezwa Uwanja wa Namfua mkoani Singida leo, Simba yenye pointi 88, inahitaji ushindi ambao utaiwezesha kufikisha alama 91 ambazo haziwezi kufikiwa na klabu yoyote kwenye msimamo wa ligi hiyo msimu huu.

Hata hivyo, Yanga inayoshika nafasi ya pili kwenye msimamo wa ligi hiyo, endapo itashinda michezo yake miwili iliyosalia itafikisha alama 89, wakati huu Simba ikiwa na mechi tatu mkononi pamoja na mechi hiyo ya leo.

Mabingwa hao watetezi, msimu uliopita pia walitwaa ubingwa wa ligi hiyo wakiwa Singida, tena siku moja kabla ya mchezo baada ya watani zao, Yanga kutoka sare dhidi ya Tanzania Prisons.

Aussems, aliliambia Nipashe jana kuwa, timu yake inahitaji kushinda mechi zote tatu za ligi hiyo zilizobaki na si mchezo mmoja wa leo kama ambavyo inaonekana.

Aussems alisema kuwa nguvu waliyotumia wakati wanaanza msimu huu ndiyo wataendelea nayo mpaka katika mchezo wa mwisho ambao utakuwa ni dhidi ya Mtibwa Sugar utakaochezwa Jumanne kwenye Uwanja wa Jamhuri, Morogoro.

"Mashabiki wa Simba tuifanye Singida kuwa mji wetu wa kusherehekea kikombe cha ubingwa," alisema kwa kifupi kocha huyo raia wa Ubelgiji.

Meneja wa Simba, Patrick Rweyemamu, alisema kikosi chao kilifika salama Singida jana mchana kwa kutumia usafiri wa ndege kutoka Dar es Salaam hadi Dodoma na baadaye kutumia basi maalumu la kukodi kwenda mkoani humo.

Rweyemamu aliwataja wachezaji watakaokosekana katika mchezo wa leo ambao wamebaki jijini Dar es Salaam kuwa ni pamoja Zana Coulibaly, Said Ndemla na Mohammed Ibrahim "Mo".

Singida United itashuka uwanjani ikiwa na kumbukumbu ya kutoka sare zinazofanana za mabao 2-2 mara mbili mfululizo, dhidi ya Stand United na  JKT Tanzania, wakati Simba imeshinda michezo yake dhidi ya Mtibwa Sugar na Ndanda FC.

Habari Kubwa