Azam, Abalora waachana, Awesu ndani

01Aug 2020
Saada Akida
Dar es Salaam
Nipashe
Azam, Abalora waachana, Awesu ndani

UONGOZI wa Azam FC umesema wameachana rasmi na kipa wao namba moja, Razak Abalora na sasa wapo katika mazungumzo na mlinda mlango kutoka ndani ya nchini.

Mtendaji Mkuu wa Azam FC, Abdulkarim Amin 'Popat' (kulia), akimtambulisha kiungo Awesu Awesu juzi, baada ya kumsajili kama mchezaji huru kutokana na kumaliza mkataba na Kagera Sugar. NA MPIGAPICHA WETU

Akizungumza na gazeti hili jijini Dar es Salaam jana, Mtendaji Mkuu wa timu hiyo, Abdulkarim Amin 'Popat', alisema wameachana na kipa huyo baada ya mkataba wake kufika tamati.

Alisema Abarola hawatamuongezea mkataba na wapo katika mchakato wa kuzungumza na kipa kutoka ndani ya nchi atayeongeza nguvu katika kikosi cha timu hiyo.

"Tumeanza usajili kwa kumnasa kiungo kutoka Kagera Sugar, Awesu Awesu kwa mkataba wa miaka miwili kuanzia sasa ni mchezaji halali, tumemsajili kwa kufuata mapendekezo ya kocha wetu, Aristica Cioaba.

Awesu ni miongoni mwa majina 12 ambayo yaliingia katika mchujo hadi kufikia matano na hatimaye kuvutiwa na kiwango cha nyota huyo," alisema Popat.

Alisema mbali na huyo pia muda wowote kuanzia sasa wataendelea kusainisha mikataba wachezaji wao wapya walioafikiana, baada ya kocha kuhitaji kujenga kikosi kipana.

"Kocha anahitaji kuwa na kikosi kipana, hivyo ametaka tusajili winga wa kulia na kushoto, mabeki wote wawili na mshambuliaji mzuri, msimu huu safu ya ushambuliaji haikuwa bora," alisema Popat.

Wakati huo huo, kiungo mpya wa Azam, Awesu ameahidi kufanya makubwa na yenye mafanikio kushirikiana na wachezaji wenzake ndani ya timu hiyo kwa msimu mpya wa Ligi Kuu Tanzania Bara.

Alisema aliwahi kucheza Azam katika kikosi cha vijana kabla ya kuondoka na sasa amefurahi kurejea katika timu yake hiyo kuifanyia makubwa.

"Hakuna mchezaji ambaye hapendi kuja kucheza ndani ya Azam, ni klabu kubwa, nimerejea kufanya kazi ambayo niliianza, nina imani nitazidi kupambana ili kuwa bora zaidi," alisema Awesu.

Kiungo huyo juzi amesaini mkataba wa miaka miwili kuitumikia Azam FC akiwa ni mchezaji huru baada ya dili lake na Kagera Sugar kufika tamati.

Habari Kubwa