Azam: Bado tuna nafasi kuivua ubingwa Yanga

26Feb 2016
Sanula Athanas
Dar
Nipashe
Azam: Bado tuna nafasi kuivua ubingwa Yanga
  • Timu hiyo ya Chamazi ililazimishwa suluhu na Prisons juzi huku Erasto Nyoni akilimwa kadi ya njano na kumfanya akose mechi ijayo dhidi ya Yanga.

KOCHA wa Azam FC, Stewart Hall, amesema suluhu waliyoipata dhidi ya Tanzania Prisons juzi si tatizo kwa kuwa bado wapo kwenye vita ya kuivua Yanga ubingwa wa Ligi Kuu Tanzania Bara msimu huu.

Kocha wa Azam FC, Stewart Hall.

Mabingwa hao wapya wa Afrika Mashariki na Kati wamefanikiwa kuchukua pointi nne kati ya sita mjini Mbeya msimu huu wakishinda 3-0 dhidi ya Mbeya City kabla ya juzi kubanwa na maafande hao ambao wamekusanya pointi tano kutoka timu za '3-bora' wakiitwanga Simba bao 1-0 kabla ya kuishika Yanga kwa sare ya magoli 2-2.

Azam bado inakamata nafasi ya pili ikiwa na pointi 46 baada ya mechi 19 sawa na vinara Yanga, zote zikizidiwa mchezo mmoja na Simba inayoshika nafasi ya tatu ikiwa na mtaji wa pointi 45.

Na Hall anaamini Azam FC bado ina nafasi ya kutwaa taji la pili la ligi ya Bara kwa kuwa watacheza dhidi ya Yanga Machi 5 na wana faida ya mchezo mmoja mkononi dhidi ya Simba.

"Prisons ni timu inayotumia nguvu sana, walifanya rafu kadhaa mbaya nyingine kwa viwiko na wakati mwingine tukiwa hatuna mpira, nadhani mwamuzi hakuwa na ubora unaotakiwa, nafikiri angewapa kadi za njano mapema ili kutuliza aina ya uchezaji wao, lakini hakufanya hivyo," Hall alikaririwa na mtandao rasmi wa Azam FC jana.

"Tulijitahidi kama timu kucheza kwa nguvu, tulipambana kwa nguvu sana kusaka ushindi, lakini hakuna aliyeshinda hapa (Mbeya), Simba alikuja hapa alifungwa (1-0), Yanga naye alilazimisha sare dakika za mwisho kwa kupewa penalti.

"Pia tulinyimwa penalti ya wazi baada ya (Shomari) Kapombe kuangushwa ndani boksi, ninafikiri tungeweza kuimaliza mechi ndani ya kipindi cha kwanza kwa kushinda. Kipindi cha pili walipoteza sana muda, hawakuwa na nia ya kushinda na walitumia kila mbinu kutuzuia tusishinde."

NYONI KUIKOSA YANGA
Kiungo mkabaji anayechezeshwa kama beki wa kati wa kwa sasa katika mfumo wa Azam FC wa 3-5-2, Erasto Nyoni, alionywa kwa kadi ya njano juzi kutokana na kukoromeana na mmoja wa wachezaji wa Prisons ikiwa ni kadi yake ya tatu ya njano kulimwa msimu huu, hivyo kulazimika kuikosa mechi ijayo dhidi ya Yanga.

"Niliongea na wachezaji kuhusiana na aina ya kadi hizo kabla ya mchezo, lakini nimeshangaa kutokea na sasa ataikosa mechi ya Yanga, Nyoni amecheza vema sana akiwa na mabeki wengine wawili wa kati, Pascal Wawa na David Mwantika, ndani ya mechi mbili zilizopita hatujaruhusu bao, sasa nalazimika kubadilisha safu ya ulinzi kuelekea mechi ijayo dhidi ya Yanga, tunamshukuru Mungu Aggrey Morris anarejea," Hall alisema.

"Baada ya kuona hali hiyo, nililazimika kumtoa John Bocco ili kumwepusha asikose mechi ya Yanga, hasa baada ya kuona kuwa kuna kila dalili za mwamuzi kumwonyesha kadi ya njano," alisema.

Kikosi cha Wanalambalamba kilirejea jijini Dar es Salaam jana saa 3 asubuhi kwa 'pipa' kujipanga kwa mechi ya Kombe la Kombe la Shirikisho dhidi ya Panone FC itakayochezwa kwenye Uwanja wa Ushirika mjini Moshi Jumatatu.

Habari Kubwa