Azam: CAF basi, akili kwa Yanga

25Oct 2021
Saada Akida
Dar es Salaam
Nipashe
Azam: CAF basi, akili kwa Yanga

BAADA ya kutolewa katika michuano ya Kombe la Shirikisho Afrika, Kocha Msaidizi wa Azam FC, Vivier Bahati, amesema akili na nguvu zote sasa wanazihamishia katika michezo yao ya Ligi Kuu Tanzania Bara ukiwamo ule wa Oktoba 30, mwaka huu dhidi ya Yanga.

Azam juzi ilitolewa katika michuano hiyo ya kimataifa kwa kukubali kipigo cha bao 1-0 ugenini dhidi ya Pyramids ya Misri ikiwa ni baada ya kutoka suluhu katika mchezo wa kwanza nyumbani.

Akizungumza na gazeti hili jana kwa simu, Vivier alisema wamepokea matokeo hayo na sasa wanarejea nyumbani kujipanga kwa michezo iliyopo mbele yao ikiwamo ya Ligi Kuu na Kombe la FA.

Alisema mechi ilikuwa ya ushindani mkubwa na baada ya kufungwa walilazimika kuanza kutafuta bao la kusawazisha, lakini hawakuwa na bahati, sasa nguvu wanazihamishia kwenye mchezo dhidi ya Yanga.

"Ulikuwa mchezo mzuri tulijitahidi kupambana kwa ajili ya kupata matokeo, lakini tumeshindwa kufikia malengo sasa tunarudi nyumbani kupambana katika ligi, tunahitaji, kupambana na kufanya vizuri mechi zetu za nyumbani," alisema Vivier.

Alisema baada ya kushindwa kufikia malengo yao ya kucheza hatua ya makundi ya CAF, sasa wanarejea kuhakikisha wanapambana kutafuta matokeo mazuri katika michezo yao ya ligi wakianza na uliopo mbele yao dhidi ya Yanga.

Habari Kubwa