Azam FC, Bidvest Wits kucheza mchana jua kali

17Mar 2016
Na Mwandishi Wetu
Nipashe
Azam FC, Bidvest Wits kucheza mchana jua kali

LICHA ya kupata ushindi mnono wa magoli 3-0 katika mechi ya kwanza iliyofanyika ugenini, Azam FC imepanga kuibamiza tena Bidvest Wits kwa kuikabili mchana jua kali katika mechi yao ya pili ya michuano ya Kombe la Shirikisho barani Afrika.

Mabao ya Salum Abubakar, John Bocco na Shomari Kapombe yaliwang'arisha Wanalambalamba ugenini mwishoni mwa wiki iliyopita, lakini wameamua kucheza mechi ya marudiano Jumapili kuanzia saa 9:15 mchana kwenye Uwanja wa Azam jijini Dar es Salaam. Muda huo kunakuwa na jua na joto kali jijini.

Ofisa Mtendaji Mkuu wa Azam FC, Saad Kawemba, alisema jana kuwa benchi lao la ufundi linaloongozwa na Mwingereza Stewart Hall, ndilo limependekeza muda huo wa kuanza kwa mchezo na wanaamini utakuwa na faida kubwa kwa wenyeji.

Kiongozi huyo aliongeza wakiwa Johannesburg, Afrika Kusini, walicheza na kufanya mazoezi katika mazingira ya baridi hali ambayo ni tofauti na hapa jijini. Na hii ni "neema kwa Azam FC".

Aliongeza kuwa wapinzani wao watawasili nchini Jumamosi wakiwa na msafara wa watu 30 (wachezaji 22).

Habari Kubwa