Azam FC: Hesabu CAF bado ngumu

13Sep 2021
Saada Akida
Dar es Salaam
Nipashe
Azam FC: Hesabu CAF bado ngumu

LICHA ya kuanza na ushindi wa mabao 3-1 dhidi ya Horseed SC ya Somalia, Kocha Msaidizi wa Azam FC, Vivier Bahati, amesema hilo haliwapi uhakika wa kusonga mbele katika michuano ya Kombe la Shirikisho Afrika na kwamba wanahitaji kupambana zaidi ili kushinda katika mchezo wa marudiano.

Mabao ya Azam katika mchezo huo yalifungwa na Ayoub Lyanga, Idris Mbombo na Lusajo Mwaikenda ambapo walitoka nyuma kwa bao 1-0 na kupindua meza kwa ushindi huo mnono.

Akizungumza baada ya mchezo huo, Bahati alisema amefurahishwa na matokeo hayo licha ya kuanza kipindi cha kwanza wakiwa chini ila baada ya mapumziko vijana wao walipambana na kupata matokeo hayo chanya.

“Kipindi cha kwanza hatukucheza vizuri ila nawapongeza vijana wangu kwani kipindi cha pili walikuwa na morali na kufanikiwa kupata mabao mawili baada ya kuingia na mpango wetu kwa kutumia ubora na mapungufu yao," alisema Bahati.

Kuhusu mchezo wa marudiano utakaochezwa katika ardhi ya Tanzania tena, alisema ni faida kwao na ana matumaini katika mpira wa kisasa hakuna nyumbani au ugenini, hivyo wanachotakiwa ni kupata matokeo.

“Faida tutakayoipata ni kuto kusafiri, mpira wa kisasa hakuna cha nyumbani wala ugenini kokote unaweza pata matokeo cha kufanya ni kupambana na kuwasisitiza wachezaji kutobweteka na matokeo ya mechi hii," alisema Bahati.

Kwa upande wa Kocha Mkuu wa Horseed, Mohammed Hussein, licha ya kupoteza kwa mabao 3-1, amewapongeza wachezaji wake kwa kile walichokionyesha kwani walijua wanacheza na timu kubwa.

“Azam ni timu kubwa na tangu tunatoka Somalia tulijua tunaenda kucheza na timu kubwa na niwapongeze vijana wangu kwa kucheza vizuri licha ya kwamba tulifungwa,” alisema Hussein.

Alisema kwa sasa atatumia muda uliobaki kurekebisha makosa aliyoyaona mfano katika mipira ya kutenga ili kujiweka sawa na mchezo wa marudiano Jumamosi wiki hii.

Habari Kubwa