Azam FC kama Yanga

21Mar 2016
Somoe Ng'itu
Nipashe
Azam FC kama Yanga
  • ***Ni baada ya timu hiyo kufuzu hatua inayofuata ya Kombe la Shirikisho Afrika

AZAM FC sasa itakumbana na timu ya Esperance ya Tunisia katika mechi inayofuata ya Kombe la Shirikisho baada ya jana kuifunga Timu ya Bidvest Wits kutoka Afrika Kusini kwa mabao 4-3 kwenye Uwanja wa Chamazi, Dar es Salaam.

Kwa ushindi huo, Azam inasonga mbele kwa jumla ya mabao 7-3, baada ya kushinda mchezo wa kwanza ugenini kwa mabao 3-0.

Straika wa kimataifa wa Azam FC kutoka Ivory Coast, Kipre Tchetche alikuwa wa kwanza kuipatia timu yake bao dakika ya 22 akimalizia krosi ya Ramadhani Singano.

Nahodha John Bocco aliongeza bao la pili katika dakika ya 42 akimalizia pasi ya Kipre Tchetche, kabla ya wageni kufunga bao la kwanza kupitia kwa Jabulani Shongwe aliyepiga shuti la kushtukiza nje ya 18 na kumshinda kipa Aishi Manula.

Tchetche alifunga bao la tatu katika dakika ya 58 baada ya kupokea pasi kutoka kwa kiungo Salum Aboubakar, kabla ya Bidvest Wits kufunga bao la pili kupitia kwa Mosiatlhaga Kosiekante.Tchetche alikamailisha furaha kwa kufunga 'hat trick', likiwa bao la nne kwa Azam.

Wageni, ambao walichezesha wachezaji wengi wa kikosi cha pili, walipunguza machungu ya kipigo kwa kufunga bao la tatu katika dakika ya 89 kupitia kwa Botes Henrico.

Habari Kubwa