Azam FC kuanza ratiba ngumu ugenini leo

14Feb 2016
Faustine Feliciane
Nipashe Jumapili
Azam FC kuanza ratiba ngumu ugenini leo

KLABU ya Azam FC, leo inaanza ratiba ngumu ya kucheza michezo mitano nje ya uwanja wake wa nyumbani, Chamazi nje kidogo ya jiji la Dar es Salaam.

wachezaji timu ya Azam

Azam leo inapambana na Coastal Union kwenye Uwanja wa Mkwakwani katika mchezo wa Ligi Kuu Bara, ambao ni moja wapo kati ya mitano watakayocheza nje ya Chamazi pamoja na mchezo wa Kombe la Shirikisho (FA) dhidi ya Panone FC kwenye Uwanja wa Ushirika mjini Moshi utakaochezwa Februari 28.

Kocha wa Azam, Stewart Hall alisema kikosi chake kinakabiliana na changamoto ya ratiba, lakini watapambana na kushinda mechi zote za ratiba ya ugenini.

"Ukiangalia ratiba imetubana sana, lakini tumejipanga kuhakikisha tunafanya vizuri katika michezo yote tukianza na mchezo wa kesho (leo) dhidi ya Coastal," alisema Hall. Kuhusu mechi dhidi ya Coastal, alisema utakuwa mchezo mgumu kwani wapinzani wao watakuwa kwenye uwanja wa nyumbani. "Yanga walifungwa Mkwakwani, hivyo timu hii siyo rahisi.

Lazima wamejiandaa vizuri kushinda mchezo wa leo," alisema Hall. Ratiba inaonyesha mara baada ya mchezo wa leo, Azam itaelekea Mbeya kucheza na Mbeya City Jumamosi ijayo kwenye Uwanja wa Sokoine, siku nne baadaye watacheza na Tanzania Prisons (Februari 24) kwenye uwanja huohuo.

Baada ya hapo itaelekea mjini Moshi kucheza na Panone FC kwenye mchezo wa Kombe la Shirikisho Februari 28, kabla ya kurejea Dar es Salaam kucheza na Yanga kwenye Uwanja wa Taifa, Machi 5. Mchezo wa mwisho wa Azam kucheza kwenye uwanja wake wa nyumbani ilikuwa dhidi ya Mwadui FC Jumapili iliyopita na kuibuka na ushindi wa bao 1-0.

Habari Kubwa