Azam FC kuwamalizia Waethiopia Chamazi

13Aug 2019
Na Mwandishi Wetu
Dar es Salaam
Nipashe
Azam FC kuwamalizia Waethiopia Chamazi

LICHA ya kukubali kipigo cha bao 1-0 dhidi ya Fasil Kenema kwenye mchezo wa kwanza wa michuano ya Kombe la Shirikisho Afrika, Azam FC imeahidi kufanya kweli katika mechi ya marudiano itakayopigwa jijini Dar es Salaam Agosti 24, mwaka huu.

uwanja wa azam fc chamanzi.

Azam imekuwa timu pekee iliyopoteza kati ya nne zinazopeperusha bendera ya nchi kwenye michuano ya kimataifa kwa upande wa Tanzania Bara.

Azam FC inayonolewa na Mrundi Etienne Ndayiragije ikiwa ugenini nchini Ethiopia juzi, ilikubali kipigo cha bao 1-0 katika mchezo uliokuwa na presha kali kutokana na wenyeji kupata sapoti kubwa kutoka kwa mashabiki wao walioujaza uwanja wao unaokadiriwa kuchukua watazamaji 55,000 kutokana na kuruhusiwa kuingia bure.

KMC ambayo inashiriki michuano ya Kombe la Shirikisho yenyewe Jumamosi ilifanikiwa kupata sare tasa ugenini Kigali dhidi ya AS Kigali,  wakati Simba na Yanga zinazopeperusha bendera ya nchi kwenye michuano ya Ligi ya Mabingwa Afrika nazo zikitoka sare katika mechi zao za awali.

Simba ikiwa ugenini Msumbiji, ilitoka sare tasa dhidi ya UD Songo wakati Yanga ikilazimishwa sare ya bao 1-1 nyumbani katika Uwanja wa Taifa dhidi ya Township Rollers ya Botswana.

Afisa Habari wa Azam FC, Jaffary Maganga akizungumza baada ya mechi hiyo kumalizika juzi, alisema dakika 90 za mwanzo zimekamilika kwa kupoteza, hivyo hesabu zao ni kujipanga kupata matokeo chanya mechi ya nyumbani.

"Tumemaliza dakika 90 za awali ugenini, baada ya kumaliza kwa kufungwa bao 1-0, sasa mipango yetu ni mchezo wa marudio na sisi tutatumia vema uwanja wa nyumbani ili kusonga mbele," alisema.

Azam sasa itabidi kuhamasisha mashabiki wengi kwenda uwanjani kuipa sapoti itakaporudiana na timu hiyo katika Uwanja wa Azam Complex Agosti 24 ili kuweza kupata matokeo.

Mshindi wa jumla katika mechi hiyo atamenyana na mshindi kati ya Triangle FC ya Zimbabwe na Rukinzo FC ya Burundi, anapotokea kocha Ndayiragije.

Habari Kubwa