Azam FC siku 280 bila kupoteza mechi VPL

09Feb 2016
Sanula Athanas
Dar es Salaam
Nipashe
Azam FC siku 280 bila kupoteza mechi VPL

AZAM FC wanatisha! Ndivyo unavyoweza kusema baada ya timu hiyo kucheza mechi 18 mfululizo za Ligi Kuu ya Vodacom Tanzania Bara (VPL) bila kupoteza hata moja.

Azam FC

Goli la video lililofungwa na straika wa kimataifa kutoka Ivory Coast baada ya pasi sita kupigwa ndani ya sekunde tatu kwenye lango la Mwadui FC jijini Dar es Salaam liliipa Azam FC ushindi wa 13 msimu huu na wa 14 tangu walipopoteza mechi yao ya mwisho ya ligi hiyo msimu uliopita walipolala 2-1 dhidi ya Simba kwenye Uwanja wa Taifa Mei 3, 2015. Kwa mantiki hiyo, kikosi cha Mwingereza Stewart Hall, kimekaa siku 280 (tangu Mei 3, 2015 hadi Februari 7 mwaka huu) bila kupoteza mechi ya Ligi Kuu kikifunga mabao 33 (31 msimu huu, mawili katika ushindi wa 2-1 dhidi ya Yanga Mei 6 mwaka jana kabla hawatoka suluhu nyumbani dhidi ya Mgambo Shooting kwenye mechi yao ya mwisho msimu uliopita). Katika mechi zote hizo 18, kipa shujaa wa penalti, Aishi Manula, ndiye aliyekuwa kwenye lango la Azam FC akiruhusu mabao 11 (10 msimu huu) huku akipangua matuta yote matatu yaliyotolewa dhidi ya timu yake msimu huu dhidi ya Mwadui FC, Yanga na Kagera Sugar. Azam wamepewa penalti moja msimu huu, nahodha John Bocco akifunga katika ushindi wao wa mabao 4-2 dhidi ya JKT Ruvu kwenye Uwanja wa Karume jijini Dar es Salaam Oktoba 29.

Habari Kubwa