Azam FC wabembeleza mfumo wao

10Feb 2016
Sanula Athanas
Nipashe
Azam FC wabembeleza mfumo wao

LICHA ya kufunga mabao matano katika mechi nne zilizopita za Ligi Kuu Bara na kukusanya pointi 10, Azam FC wamesema hawana mpango wa kubadili mfumo wao wa uchezaji.

Tangu Mwingereza Stewart Hall arejeshwe Chamazi kwa mara ya pili msimu uliopita, mabingwa hao wa msimu wa 2013/14 wamekuwa wakitumia mfumo wa 3-5-2 uliowapa taji la Klabu Bingwa Afrika Mashariki na Kati mwaka jana.

Hata hivyo, katika siku za karibuni mfumo huo umeonekana kushtukiwa na timu nyingi zinazoshiriki ligi hiyo kutokana na kupungua kwa magoli yanayofungwa na kikosi cha Wanalambalamba.

Kocha Msaidizi wa Azam FC, Dennis Kitambi, alisema jana kuwa tatizo la timu yao kwa sasa sio mfumo kama inavyodhaniwa na wengi, bali kuna 'baadhi ya vitu vidogo'.

“Si jambo jepesi kubadilisha mfumo hivi sasa na kuanza kutumia mwingine, ikumbukwe ya kuwa mfumo huu tumeanza kuufanyia kazi tangu Juni mwaka jana.

“Kama nilivyosema, kuna baadhi ya vitu ndio vinatakiwa kufanyiwa kazi, kama ulivyoona katika mechi iliyopita (dhidi ya Mwadui FC) tulitengeneza nafasi takribani sita hadi saba za kufunga kipindi cha kwanza, lakini tumeshindwa kuzitumia,” alisema.
Katika mechi nne zilizopita Azam imeruhusu mabao matatu, huku ikifunga matano dhidi ya Mwadui FC (1-0), Mgambo Shooting (2-1), African Sports (1-1) na Mtibwa Sugar (1-0).

Timu hiyo inayokamata nafasi ya tatu kwenye msimamo, Jumapili itakuwa kwenye Uwanja wa Mkwakwani, Tanga kuwakabili Coastal Union ambao wameshindwa kupata pointi hata moja katika mechi mbili zilizopita dhidi ya Ndanda FC na Toto Africans tangu walipoifunga Yanga mabao 2-0.

Kikosi cha Stewart kitatinga kwenye Uwanja wa Mkwakwani kikiwa na rekodi nzuri ya kuwa timu pekee ambayo haijapoteza mechi hadi sasa na haijaacha pointi ugenini.

Habari Kubwa