Azam FC wapata kauli sare Simba

15May 2019
Somoe Ng'itu
DAR ES SALAAM
Nipashe
Azam FC wapata kauli sare Simba

BAADA ya timu yake kuambulia pointi moja kutoka kwa Simba msimu huu, Kocha Msaidizi wa Azam FC, Iddi Cheche, amesema mvua iliyonyesha juzi jijini Dar es Salam imemharibia mipango yake ya kuibuka na ushindi katika mchezo wa Ligi Kuu Tanzania Bara uliowakutanisha kwenye Uwanja wa Uhuru.

Kocha Msaidizi wa Azam FC, Iddi Cheche.

Katika mechi ya mzunguko wa kwanza Azam FC ikiwa chini ya Mholanzi Hans van der Pluijm ilichapwa mabao 3-1.

Akizungumza na gazeti hili baada ya mechi hiyo juzi, Cheche alisema amehuzunishwa na kitendo cha kugawana pointi na Simba, kwa sababu timu yake ilikuwa bora na ilistahili kupata ushindi katika mchezo huo.

Cheche alisema aliwaandaa vema wachezaji wake kuwabana nyota wa Simba na mara zote anapokabidhiwa kikosi hicho hupata matokeo mazuri.

"Mvua iliharibu mchezo, wachezaji wameshindwa kufanyia vema yale tuliyotarajia kwa sababu hali ya maji uwanjani ilisumbua, napenda niseme nimepoteza pointi mbili, haikuwa matarajio yangu," alisema kocha huyo kiraka ambaye ni maalum kwa kuandaa wachezaji wa U-20 wa matajiri hao wa Chamazi.

Naye beki kisiki na nahodha wa Azam FC, Aggrey Moris aliliambia gazeti ili kuwa mechi ilikuwa ngumu kwa kila timu na hiyo ilitokana na kila upande kuundwa na wachezaji wenye uzoefu na wakakamavu.

Alisema walijipanga kulipiza kisasi na hiyo iliwasaidia kutoruhusu bao lolote kufungwa na wapinzani wao.

Azam yenye pointi 69 imebakiza mechi mbili ili kumaliza msimu huu, lakini ikiwa inasubiri kuwavaa Lipuli FC katika mechi ya fainali ya mashindano ya Kombe la FA itakayochezwa Juni Mosi kwenye Uwanja wa Ilulu mkoani Lindi.

Habari Kubwa