Azam FC yaanza na mguu wa kulia

11Apr 2016
Na Waandishi Wetu
Dar
Nipashe
Azam FC yaanza na mguu wa kulia
  • ***Ni baada ya kupata ushindi katika mechi ya kwanza Kombe la Shirikisho Afrika dhidi ya Esperance ya Tunisia...

AZAM FC, jana ilipiga hatua moja ya mguu wa kulia kuelekea katika michuano ya Kombe la Shirikisho baada ya kutoka nyuma kufungwa bao na kuibuka na ushindi wa mabao 2-1 dhidi ya Esparance ya Tunisia katika mechi ya kwanza ya mashindano hayo iliyopigwa kwenye Uwanja wa Azam, Chamazi, Dar es Salaam.

Matoke hayo yanafungua nafasi ya timu hiyo angalau kusonga mbele kwenye mechi ya marudiano, kwani sasa itahitaji sare aina yoyote.

Katika mechi hiyo iliyojaa ushindani, wageni walikuwa wa kwanza kulitia kasheshe lango la wenyeji wao kwa mashambulizi ya mara kwa mara.

Hata hivyo, Esperance, moja ya timu zenye mafanikio kwenye michuano ya klabu Afrika, walilazimika kusubiri hadi dakika ya 33 kufunga bao la kuongoza.

Bao hilo lilifungwa na Haithem Jouini aliyeunganisha kwa kichwa mpira wavuni kutokana na krosi ya Iheb Mbaarki na bao hilo kudumu hadi mapumziko.

Azam FC wangeweza kusawazisha bao hilo kipindi cha kwanza kama siyo kupoteza nafasi nyingi za kufunga.
Mshambuliaji tegemeo Azam kutoka Ivory Coast, Kipre Tchetche alishindwa kufunga bao kipindi cha kwanza baada kupaisha juu mpira akiwa ndani ya eneo la hatari la Esperance.

Esperance nao walikaribia kufunga baada ya shambulizi la Fakhreddine Ben Youssef na kuokolewa na beki wa Azam.

Farid Mussa aliwaamcha mashabiki wa Azam jukwaani baada ya kufunga bao la kusawazisha kwa shuti kali la pembeni mwa lango la Esperance na kumshinda kipa Moez ben Cherifa katika dakika ya 68.

Dakika moja baada ya bao hilo, Ramadhan Singano aliifunga bao la pili linaloifanya Azam kwenda Tunisia ikiwa na faida.
Nyota huyo aliyesajiliwa kutoka Simba, aliunganisha kwenye kamba krosi ya mshambuliaji Tchetche.
Timu hizo sasa zitarudiana Aprili 20, mjini Tunis, nchini Tunisia.

Kikosi Azam FC: Aishi Manula, Erasto Nyoni, Waziri Salum, Aggrey Morris, Pascal Wawa, Jean Baptiste Mugiraneza 'Migi', Kipre Tchetche, Kipre Bolou, Ramadhan Singano 'Messi', John Bocco na Farid Mussa.

Imeandikwa na Someo Ng'itu na Renatha Msungu

Habari Kubwa