Azam FC yaknusha kuachana na Chirwa

22Jul 2021
Adam Fungamwango
Dar es Salaam
Nipashe
Azam FC yaknusha kuachana na Chirwa

HUKU ikiwa katika mchakato wa kuimarisha kikosi chake kwa kusajili wachezaji nyota kutoka sehemu mbalimbali, uongozi wa Azam FC umesema bado haujaachana na mshambuliaji wake raia wa Zambia, Obrey Chirwa.

Azam FC imelazimika kutoa kauli hiyo baada ya kuwapo kwa taarifa za kuachwa kwa mshambuliaji huyo wa zamani wa Yanga pamoja na Mghana Yakubu Mohammed, Ally Niyonzima na Mkongomani Mopiana Mozinzi.

Ofisa Mtendaji Mkuu wa Azam, Abdulkarim Amin 'Popat', amesema muda ukifika na kwa kufuata taratibu, klabu hiyo itatangaza wachezaji itakaowaacha baada ya kufuata mapendekezo ya benchi la ufundi.

Popat alisema wanahitaji kuwa na kikosi imara kwa ajili ya msimu ujao, hivyo mchakato wa kusajili kikosi kipya wanaufanya kwa umakini zaidi.

"Ni kweli ukisajili ni lazima baadhi ya wachezaji waondoke, lakini mpaka sasa Azam FC bado hatujatangaza mchezaji tuliyemwacha," alisema Popat.

Tayari Azam FC imeshawasajili wachezaji wawili wa kigeni ambao ni Wazambia, Rodgers Kola akitoka katika klabu ya Zanaco pamoja na Charles Zulu aliyekuwa akiichezea klabu ya Cape Town City ya Afrika Kusini.

Nyota mwingine aliyesajiliwa katika kikosi hicho kilichomaliza msimu uliopita kwenye nafasi ya tatu ni beki wa kushoto, Edward Charles kutoka Ruvu Shooting ya Mlandizi mkoani Pwani.

Azam iliyomaliza nafasi ya tatu kwenye Ligi Kuu, itashiriki mashindano ya kimataifa ya Kombe la Shirikisho msimu ujao ambapo kwa mujibu wa kalenda ya Shirikisho la Soka Afrika (CAF), michuano hiyo itaanza mapema Septemba.

Timu nyingine zitakazoshiriki mashindano ya kimataifa mwakani ni pamoja na mabingwa wa Ligi Kuu Tanzania Bara, Simba, Yanga iliyomaliza ya pili na Biashara United kutoka Musoma mkoani Mara.

Habari Kubwa