Azam FC yalia kukosa bahati

01Nov 2020
Saada Akida
DAR ES SALAAM
Nipashe Jumapili
Azam FC yalia kukosa bahati

KOCHA Msaidizi wa Azam FC, Vivier Bahati, amesema timu yake haikuwa na bahati ya kuondoka na ushindi katika mechi ya Ligi Kuu Bara dhidi ya JKT Tanzania iliyochezwa juzi usiku na kumalizika kwa sare ya bao 1-1.

Vivier aliliambia gazeti hili washambuliaji wake hawakuwa makini katika kutumia vyema nafasi walizozipata katika mchezo huo wa raundi ya tisa.

Kocha huyo alisema timu yao ilicheza vizuri na kuwazidi wapinzani wao lakini amekiri bahati haikuwa upande wao kwa siku ya juzi.

"Kasi ya mechi saba zilizopita ilikuwa juu sana kulingana na wapinzani ambao tumekutana, isipokuwa mechi ya nane na tisa matokeo hayakuwa mazuri kwa sababu ya upungufu yetu, hasa katika kumalizia nafasi za mwisho tunazozipata.

"Baada ya kupoteza pointi nne, sisi benchi la ufundi na wachezaji wa ujumla kila mechi tunaichukulia kama fainali yetu, ni jukumu letu kuandaa vizuri kila kitu ili kuhakikisha timu inapata pointi tatu, tunaheshimu kila tutakayekutana naye katika ligi hii,” alisema Vivier.

Naye kiungo wa timu hiyo, Salum Aboubakar 'Sure Boy', alisema miaka yote kikosi chao huwa na wakati mgumu wanapokutana na JKT Tanzania na katika mechi hiyo walikutana na ushindani mkubwa.

“Tunashukuru Mungu kupata pointi muhimu, tumefanya makosa wenzetu wameyatumia na kuanza kupata bao lakini na sisi tumetumia makosa yao kusawazisha, ligi bado ndefu tuna imani ya kufanya vizuri mechi zijazo pia kuna upungufu wetu benchi la ufundi litafanyia kazi kuelekea mechi zetu zijazo,” alisema Sure Boy.

JKT Tanzania ndio walitangulia kupata bao dakika ya 43 kupitia nyota wake, Michael Aidan kwa mpira wa adhabu na dakika 78 Azam ilisawazisha kupitia Sure Bo.

Kwa matokeo hayo, Azam imeendelea kuongoza katika msimamo wa Ligi Kuu Bara ikiwa na pointi 22 baada ya kucheza mechi tisa.

Habari Kubwa