Azam hakuna kulala

12Nov 2016
Na Mwandishi Wetu
Nipashe
Azam hakuna kulala

UONGOZI wa Klabu ya Azam umesema kikosi cha timu hiyo hakitapumzika na badala yake kocha Zeben Hernandez ataendelea na programu yake kuiandaa timu kwa ajili ya mzunguko wa pili wa ligi kuu.

Kikosi cha Azam kilitarajia kurejea Dar es Salaam jana kikitokea Shinyanga kilipoenda kucheza dhidi ya Mwadui FC na kupata ushindi mnono wa magoli 4-1.

Taarifa iliyotolewa na uongozi na kuchapishwa kwenye mtandao rasmi wa klabu hiyo, kikosi cha Azam kitaendelea na mazoezi leo huku pia kikitarajia kucheza michezo ya kirafiki katika kipindi hiki ambacho ligi imesimama.

Aidha, benchi la ufundi la timu hiyo limepanga kuongeza wachezaji wapya huku pia ikitarajia kuwatema baadhi ya wachezaji ambao hawana nafasi kwenye timu hiyo.

"Hatua hiio inakuja ikiwa ni nia ya dhati kabisa ya Azam FC kutaka kufanya vizuri zaidi kwenye mzunguko wa pili wa ligi, Kombe la Shirikisho (Azam Sports Federation Cup) na michuano ya Kimataifa inayokuja kuanzia mwezi ujao na mwakani (Kombe la Kagame na lile la Shirikisho Afrika)", ilisema taarifa hiyo iliyomnukuu Kocha msaidizi wa timu hiyo, Yeray Romero.

Azam wamemaliza mzunguko wa kwanza kwa kujikusanyia pointi 25 katika michezo 15 na wanashika nafasi ya tatu nyuma ya Yanga yenye pointi 33 na Simba inayoongoza ligi ikiwa na pointi 35.

Habari Kubwa