Azam kuishusha Yanga kileleni leo?

24Feb 2016
Sanula Athanas
Dar
Nipashe
Azam kuishusha Yanga kileleni leo?
  • Timu hiyo ya Chamazi imeshinda mechi sita kati ya saba ilizocheza nje ya Dar es Salaam msimu huu, lakini inakutana na Prisons ambayo ina rekodi nzuri dhidi yao.

LIGI Kuu Tanzania Bara itaendelea leo kwa mechi moja ambayo Azam FC wanahitaji ushindi dhidi ya Prisons kwenye Uwanja wa Sokoine, Mbeya ili kuishusha Yanga kileleni.

Azam FC.

Mechi hiyo ya kiporo ya raundi ya 16, inatarajiwa kuwa na ushindani mkubwa kutokana na historia ya timu hizo pamoja na ubora wao.

Rekodi za Nipashe zinaonyesha kuwa timu hizo zimekutana mara 11 Ligi Kuu, zikitoka sare mara tano huku kila timu ikishinda mara tatu.

Azam FC, manbingwa wa Tanzania Bara 2013/14, wanaipa uzito mkubwa mechi hiyo kwa dhamira ya kutaka kurejea kileleni.

Magoli 20 yamefungwa katika mechi zote 11 walizokutana kila timu ikitupia mara 10, jambo ambalo linaongeza mvuto zaidi ya mechi ya leo.

Lakini kikosi cha Wanalambalamba kina rekodi nzuri zaidi ya mabao msimu huu, kikitupia mara 34 na kufungwa 11 katika mechi 18 zilizopita, straika Kipre Tchetche akiwa amefunga magoli tisa, John Bocco (8) na Shomari Kapombe (7).

Wenyeji Prisons wana wastani wa kufunga bao moja kwenye kila mchezo msimu huu baada ya kufunga mabao 19 katika mechi 19 zilizopita, huku ikiruhusu nyavu zap kutikiswa mara 18, staa wao akiwa ni straika Jeremiah Juma aliyetumbukiza magoli 11 mpaka sasa.

Kikosi cha Stewart kitaingia uwanjani kikiwa na kumbukumbu ya kushinda 3-0 dhidi ya Mbeya City kwenye Uwanja wa Sokoine Jumamosi na pia ushindi wa 2-1 dhidi ya Prisons kwenye Uwanja wa Azam duru la kwanza.

Kocha Hall alisema jana kuwa mechi itakuwa ngumu kutokana na ubora wa Prisons, lakini akasisitiza wamejipanga kushinda na kupanda kileleni mwa msimamo wa ligi.

“Itakuwa ni ngumu, si kazi rahisi siku zote kucheza na timu ya jeshi, Yanga walikuja hapa wakalazimisha sare baada ya kuokolewa na mwamuzi dakika za mwisho kwa kupewa penalti (2-2), Simba imepoteza hapa (1-0) dhidi yao, watataka kuendeleza hilo, lakini sisi (Azam) tumejipanga vema kupata ushindi,” alisema.

“Awali nilipanga kumchezesha (Ramadhan Singano) Messi katikati, lakini baada ya kuwaona wachezaji wa Prisons jana (juzi), nimeamua kumpa nafasi ya Michael Bolou atayesaidiana na (Jean Mugiraneza) Migi na (Salum Abubakar) Sure Boy katikati, ili kukabiliana na aina ya uchezaji wa Prisons ambayo nyota wake wana miili mikubwa."

Katika mechi hiyo, Azam inayokamata nafasi ya pili kwenye msimamo ikiwa nyuma kwa pointi moja dhidi ya vinara Yanga wenye pointi 46, itakosa huduma ya wachezaji wake watano; kiungo Himid Mao atakayekuwa akitumikia adhabu ya kukosa mchezo mmoja baada ya kukusanya kadi tatu za njano na mabeki majeruhi Aggrey Morris, Racine Diouf na Abdallah Kheri pamoja na mshambuliaji Didier Kavumbagu ambaye pia ana majeraha.