Azam kujipima na Mtibwa kesho

09Dec 2016
Na Mwandishi Wetu
Dar es Salaam
Nipashe
Azam kujipima na Mtibwa kesho

AZAM kesho inatarajia kucheza mchezo wa kirafiki wa kujipima nguvu dhidi ya Mtibwa Sugar kwenye uwanja wa Azam Complex ikiwa ni maandalizi kuelekea mzunguko wa pili wa ligi kuu.

Meneja wa Azam B Philipo Alando katikati akiwa na Kocha Mkuu wa Azam Academy, Vivek.

Meneja wa Azam, Philipo Alando, aliiambia Nipashe jana kwamba mchezo huo utaanza kuanzia majira ya 1:00 jioni.

Alando alisema kwamba mchezo huo ni maalum kwa kocha Zeben Hernandez kukipima kikosi chake kabla ya kuanza kwa mzunguko wa pili wa Ligi Desemba 17.

“Benchi la Ufundi lilipendekeza mchezo maalum wa kirafiki ili waipime timu kabla ya kuanza kwa mzunguko wa pili wa Ligi Kuu na kwa bahati nzuri tumefanikiwa kuwapata Mtibwa,” alisema Alando.

Katika mchezo huo, mashabiki wa Azam FC watapata nafasi ya kuwaona kwa mara ya kwanza wachezaji wapya waliosajiliwa kutoka Ghana, washambuliaji Samuel Afful, Daniel Agyei na Yahaya Mohammed, wanaoungana na Mghana mwenzao, beki Daniel Amoah, kiungo Jean Baptiste Mugiraneza kutoka Rwanda na Wazimbabwe wawili, winga Bruce Kangwa na mshambuliaji Francesco Zekumbawira kukamilisha idadi ya wachezaji saba wa kigeni.

Licha ya Azam FC kutopata matokeo mazuri kwenye baadhi ya mechi za mzunguko wa kwanza wa Ligi, mwanga mzuri wa makocha hao umeanza kuonekana baada ya kuiongoza timu hiyo kuandika rekodi mbalimbali ambazo huko nyuma zilishindikana kuwekwa.

Baada ya kusota miaka mitatu mfululizo bila kutwaa ubingwa na Ngao ya Jamii, hatimaye mwaka huu Azam FC chini ya makocha hao imeweza kuandika rekodi ya kubeba taji hilo kwa kuichapa Yanga kwa mikwaju ya penalti 4-1 kufuatia sare ya 2-2 ndani ya dakika 90 za mchezo huo.

Ikiwa ina rekodi mbaya huko nyuma ya kutoweza kuichapa Tanzania Prisons nyumbani kwao ndani ya Uwanja wa Sokoine (Mbeya), msimu huu imeweza kuichapa kwa mara ya kwanza (1-0) tokea ipande daraja mwaka 2008 na kuwa timu pekee iliyozoa pointi zote sita ndani ya dimba hilo msimu huu kufuatia kuichapa pia Mbeya City mabao 2-1.

Azam imemaliza mzunguko wa kwanza ikishika nafasi ya tatu kwa kuwa na pointi 25 ikizidiwa pointi10 na vinara Simba.

Itaanza mzunguko wa pili kwa kumenyana na African Lyon Desemba 18 kwenye uwanja wa Azam Complex unaomilikiwa na klabu hiyo

Habari Kubwa