Azam kuwatumia vijana Kagame Cup

28Jul 2021
Saada Akida
Dar es Salaam
Nipashe
Azam kuwatumia vijana Kagame Cup

UONGOZI wa Azam FC umeweka wazi kwamba, watatumia kikosi cha timu ya vijana kwenye michuano ya Kombe la Kagame, linalotarajiwa kuanza kutimua vumbi Agosti 15, mwaka huu jijini Dar es Salaam.

Akizungumza na gazeti hili jijini, Kocha Msaidizi wa Azam FC, Vivier Bahati alisema jana jioni walianza mazoezi kwa ajili ya maandalizi ya michuano hiyo.

Alisema hatua ya kuwatumia wachezaji vijana ni kwa sababu wanawapa muda wa kupumzika wachezaji wao waliocheza Ligi Kuu Tanzania Bara msimu huu ulioisha.

"Katika kikosi kinachokwenda kucheza kombe la Kagame, hakitakuwa na mchezaji yoyote mkubwa aliyecheza Ligi na hata wale wapya waliosajiliwa kwa ajili ya msimu ujao,” alisema.

Alisema watatumia wachezaji hao kuhakikisha wanapata uzoefu wa kucheza mechi za ushindani kulingana na wengine kupata nafasi ya kupandishwa katika kikosi cha kwanza.

Azam ni miongoni mwa timu mbili ikiwamo Yanga zilizothibitisha kushiriki michuano hiyo ya kombe la Kagame na kuchezewa katika viwanja viwili Azam Complex na Benjamini Mkapa.