Azam kuwavaa Wasomali leo bila mashabiki, Dube

10Sep 2021
Na Waandishi Wetu
Dar es Salaam
Nipashe
Azam kuwavaa Wasomali leo bila mashabiki, Dube

WAKATI wawakilishi wa Tanzania kwenye michuano ya Kombe la Shirikisho barani Afrika (CAF), Azam FC, wakishuka dimbani leo kucheza dhidi ya Horseed ya Somalia bila uwapo wa mashabiki uwanjani, pia watakosa huduma ya straika wake hatari, Prince Dube, ambaye ni majeruhi, imeelezwa.

Uongozi wa klabu hiyo, Azam FC umeweka wazi kwamba umepokea taarifa kupitia Shirikisho la Soka nchini (TFF) kutoka Shirikisho la Soka barani Afrika (CAF) juu ya kutokuwapo kwa mashabiki uwanjani kwenye mechi yao dhidi ya Horseed FC ya Somalia.

Azam FC itawakaribisha Wasomalia hao katika mchezo huo wa awali wa Kombe la Shirikisho Afrika utakaopigwa katika Uwanja wao wa Azam Complex uliopo Chamazi, Dar es Salaam.

Akizungumza na gazeti hili jijini Dar es Salaam jana, Ofisa Habari wa Azam FC, Zakaria Thabiti 'Zaka Zakazi', alisema hawana jinsi kutokana na taarifa hizo kutoka CAF, kwa sababu hali hiyo ni kutokana na changamoto za ugonjwa wa COVID-19 ambao dunia nzima inakabiliana nao kwa sasa.

Alisema kikubwa waliendelea kufanya maandalizi mazuri baada ya wachezaji wote walikuwapo kwenye majukumu ya timu za taifa kurejea kambini kwa ajili ya maandalizi ya mchezo huo dhidi ya Horseed FC.

"Wachezaji wote wamerejea kambini akiwamo nyota wa nje ambao walikuwa katika majukumu ya mataifa yao,
wanaendelea vizuri na tuko tayari kwa ajili ya kupambana kutafuta matokeo chanya dhidi ya Horseed SC," alisema Zaka.
Aidha, Zaka alisema katika mchezo huo watamkosa straika wao hatari, Prince Dube ambaye ni majeruhi kwa sasa.

"Wachezaji wote wako salama, isipokuwa kwenye mechi hiyo tutamkosa Dube, ambaye alipata majeraha tukiwa Zambia kwenye kambi wakati wa mechi za kirafiki," alisema.

Baada ya mechi hiyo, mchezo wa marudiano umepangwa kuchezwa Uwanja wa Uhuru, Dar es Salaam, saa 10:00 jioni, na utahesabiwa kuwa ni wa ugenini kwa Azam na nyumbani kwa Horseed, ambayo imeomba ufanyike hapa nchini kutokana na hali ya machafuko kwa Somalia.