Azam: Sure Boy anaitaka Yanga

06Aug 2020
Na Mwandishi Wetu
Dar es Salaam
Nipashe
Azam: Sure Boy anaitaka Yanga

HATIMAYE Klabu ya Azam imekubali yaishe kwa kuamua kuiita Yanga mezani kuzungumza dili la kumsajili kiungo wao, Abubakari Salim 'Sure Boy', baada ya mchezaji huyo kuwaeleza dhamira yake ya kutaka kuondoka kwenda kujiunga na timu hiyo ya mtaa wa Twiga na Jangwani jijini Dar es Salaam, imeelezwa.

Awali, uongozi wa Azam FC ulieleza kupokea barua kutoka Yanga ikieleza nia yao ya kuomba kufanya mazungumzo ya kumsajili Sure Boy, lakini miamba hiyo ya Chamazi, Mbagala jijini Dar es Salaam ikakataa, kabla ya jana kuridhia na kukaribisha ofa.

"Yanga walifuata utaratibu kwa kuleta barua ya kuomba kumsajili, lakini kocha mkuu (Aristica Cioaba) alisema kiungo huyo yupo kwenye mipango yake na tulipomuuliza Sure Boy alisema hana mpango wa kuondoka, ndipo tukawajibu Yanga mchezaji huyo hauzwi," alisema Ofisa Mtendaji Mkuu wa Azam FC, Abdulkarim Amin 'Popat' na kuongeza.

"Lakini jana usiku (juzi usiku), nilizungumza tena na Sure Boy naye akaniambia anataka kuondoka, hivyo tunaisubiri Yanga ije tena maana awali walipoleta barua yao tuliwaambia hauzwi."

Hata hivyo, kwa mujibu wa taarifa zilizofikia Nipashe jana muda mfupi kabla ya kwenda mitamboni, zieleza Yanga ilitarajia kupeleka ofa yao kwa ajili ya kumsajili mchezaji huyo anayeelezwa kuvutiwa sana na timu hiyo tangu utotoni.

Mapema jana alipoulizwa Mwenyekiti wa Kamati ya Ufundi wa Yanga, Dominick Albinius, kuhusu usajili wa Sure Boy, alisema kila kitu wanakifanya kwa kufuata utaratibu na kama suala hilo lipo, likikamilika litawekwa hadharani.

Yanga inataka kuziba nafasi hiyo ya kiungo mkabaji baada ya kuachana na nahodha wao Papy Tshishimbi waliyeshindwa kukubaliana katika suala la usajili.

Habari Kubwa