Azam : Tutazifunika Simba, Yanga Bara

25Nov 2018
Na Mwandishi Wetu
Dar es Salaam
Nipashe Jumapili
Azam : Tutazifunika Simba, Yanga Bara

BAADA ya kupata ushindi wa mabao 2-1 dhidi ya Ruvu Shooting na kuendelea kujiimarisha kwenye msimamo wa Ligi Kuu Tanzania Bara, uongozi wa timu ya Azam FC umesema kuwa unaelekeza nguvu zote katika mchezo wao dhidi ya Stand United.

Ofisa Habari wa Azam FC, Jaffari Maganga picha na mtandao

Mabingwa hao wa Kombe la Kagame, Azam FC sasa wana pointi 33 baada ya kucheza mechi 13 bila kupoteza wakitoa sare 3 na kushinda michezo 10, wataikaribisha Stand United kutoka Shinyanga Desemba 4 kwenye Uwanja wa Azam Complex.

Akizungumza na gazeti hili jana, Ofisa Habari wa Azam FC, Jaffari Maganga, alisema kuwa kipaumbele cha timu yake ni kupata ushindi katika kila mchezo wanaocheza na kwa kufanya hivyo wanaamini watatimiza malengo.

Maganga alisema kila mechi kwao ni fainali na wanawakumbusha wachezaji wao kutoziangalia timu nyingine zinapata matokeo ya aina gani.

"Tunajipanga kupata matokeo chanya katika kila mechi, hii ndiyo itatupa nafasi ya kutwaa ubingwa.Hesabu zetu ni kwa kila mchezo bila kujali tunacheza na nani, tuna kikosi bora, walimu wazuri hivyo tunachohitaji ni matokeo kwa ajili ya mchezo wetu ujao," alisema.

Mabingwa watetezi Simba wenye pointi 27 wako katika nafasi ya tatu kwenye msimamo wa ligi wakiwa wamecheza mechi 12 huku Yanga yenye pointi 29 ni ya pili lakini wamecheza mechi 11.

Ligi hiyo inatarajia kuendelea tena leo kwa Kagera Sugar kuikaribisha Yanga kwenye Uwanja wa Kaitaba, Bukoba.

Habari Kubwa