Azam wawatwisha 'zigo' marefa

07Mar 2016
Sanula Athanas
Nipashe
Azam wawatwisha 'zigo' marefa

BAADA ya kushikwa kwa sare ya mabao 2-2 na Yanga juzi, Azam FC wamedai marefa waliinyima timu yao ushindi katika mechi hiyo ya raundi ya 21 ya Ligi Kuu Tanzania Bara msimu huu.

kikosi cha Azam

Timu hizo zilitoka sare ya pili Ligi Kuu na ya tano katika mashindano yote msimu huu, Azam wakitangulia kuziona nyavu za Yanga kupitia kwa Juma Abdul aliyejifunga kabla ya beki huyo wa pembeni kulia kusahihisha makosa kwa goli la shuti kali na baadaye Donald Ngoma kuongeza la pili, lakini John Bocco kuwasawazishia Wanajangwani.

Kocha mkuu wa Azam FC, Stewart Hall, alimtuma msaidizi wake, Dennis Kitambi kuzungumza na waandishi wa habari juzi. Na kocha huyo wa zamani wa Ndanda FC, hakuficha kutoridhishwa kwake na uchezeshaji wa marefa.

"(Shomari) Kapombe amefunga goli (dakika ya 20) limekataliwa, tumepata penalti, lakini uamuzi unakuwa tofauti," alisema kocha huyo anayeshikilia rekodi ya kuwa kocha pekee wa Ligi Kuu msimu huu mwenye Shahada ya Uzamili (Masters).

Kocha mkuu wa Yanga, Hans van Pluijm aliwapongeza nyota wake kwa kupambana mwanzo-mwisho na kupata pointi moja dhidi ya timu hiyo ambayo hawajawahi kuchukua pointi Ligi Kuu tangu Februari 23, 2013 waliposhinda 1-0.

"Sioni haja ya kulaumu waamuzi, wapinzani wetu (Azam) wamepata nafasi nyingi za kufunga mabao mengi, lakini wametumia mbili.

Wachezaji wangu wamepambana na wamefanya kazi kubwa," alisema Mdachi huyo. Timu zote mbili zimekusanya pointi 47 katika mechi 20, Yanga ikishika nafasi ya pili kwa faida ya magoli, lakini wako nyuma kwa pointi moja dhidi ya vinara Simba ambao wamecheza mechi 21.

Habari Kubwa