Azam ya Waspaniola mechi tatu bila ushindi

14Aug 2016
Na Mwandishi Wetu
Lete Raha
Azam ya Waspaniola mechi tatu bila ushindi

AZAM FC juzi usiku imekamilisha mechi tatu za kujipima nguvu chini ya benchi lake jipya la Ufundi la makocha kutoka Hispania bila kushinda hata moja, ikitoa sare zote, mbili nyumbani na moja ugenini.

makocha wapya wa azam kutoka Hispania.

Azam FC juzi ililazimishwa sare ya 1-1 na URA ya Uganda katika mchezo wa kirafiki – shukrani kwa nahodha wake, John Raphael Bocco ‘Adebayor’ aliyesawazishia bao mwishoni mwa kipindi cha pili \Uwanja wa Azam Complex, Chamazi, Dar es Salaam.

Huo unakuwa mchezo wa tatu mfululizo Azam FC iliyo chini ya makocha kutoka Hispania inacheza bila kushinda, baada ya awali kutoa pia sare ya 1-1 na JKT Ruvu Chamazi na Ruvu Shooting Uwanja wa Mabatini, Mlandizi, Pwani.

Ikumbukwe Azam FC itamenyana na mabingwa wa mataji yote nchini, Yanga SC Agosti 17, mwaka huu katika mchezo wa Ngao ya Jamii, Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam.

Na huo utakuwa mchezo wa kwanza wa mashindano chini ya makocha wapya kutoka Hispania, Zebensul Hernandez Rodriguez anayesadiwa na Jonas Garcia Luis, Yeray Romero, Kocha wa utimamu wa mwili (Physic), Pablo Borges, Kocha wa makipa Jose Garcia na Daktari Sergio Soto Perez.

Juzi, Bocco aliifungia Azam FC bao la kusawazisha dakika ya 73 kwa penalti baada ya mchezaji aliye katika majaribio kutoka Zimbabwe, Francesco Zekumbawire kuchezewa rafu na Julius Ntambi kwenye eneo la hatari.

Wakusanya Kodi wa Uganda, URA walipata bao la kuongoza mapema tu baada ya kuanza kipindi cha pli kupitia kwa Labama Bakota aliyefunga kwa kichwa akimalizia krosi ya Shafiq Kagimu.

URA wanatarajiwa kucheza mechi yao ya pili katika ziara yao ya Tanzania Jumapili, watakapomenyana na Simba SC Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam.

Habari Kubwa